Warumi 2

Warumi 2

Hukumu ya Mungu yenye haki

1Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale.[#Mt 7:1; Lk 6:37; Yn 8:7]

2Nasi tunajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo.

3Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu?

4Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?[#2 Pet 3:15]

5Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,

6atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;[#Zab 62:12; Mit 24:12; Mt 16:27; Yn 5:29; 2 Kor 5:10]

7wale ambao kwa subira katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutoharibika, watapewa uzima wa milele;

8na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;[#2 The 1:8]

9dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Mgiriki pia;[#Rum 1:16; 3:9]

10bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Mgiriki pia;

11kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.[#Kum 10:17; Mdo 10:34; 1 Pet 1:17]

12Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria.

13Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.[#Mt 7:21; 1 Yoh 3:7; Yak 1:22,25]

14Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe.[#Mdo 10:35]

15Hao waionesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea;[#Rum 1:32]

16katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na Injili yangu, kwa Kristo Yesu.[#2 Tim 2:8]

Wayahudi na sheria

17Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu,[#Yak 2:19]

18na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati,[#Flp 1:10]

19na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani,[#Mt 15:14; Lk 18:9]

20mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati;[#2 Tim 3:5]

21basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?[#Zab 50:16-21; Mt 23:3,4]

22Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wayaibia mahekalu?

23Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

24Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa.[#Isa 52:5; Eze 36:20]

25Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutotahiriwa.[#Yer 4:4; 9:24,25]

26Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutotahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?[#Gal 5:6]

27Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaivunja torati?

28Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;[#Yn 8:15,39; 7:24]

29bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.[#Kum 30:6; Mwa 49:8; Kol 2:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya