The chat will start when you send the first message.
1Hapo zamani Waamuzi walipokuwa wanatawala, njaa ilitokea katika nchi. Mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaondoka akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili.[#Amu 2:16; Mwa 12:10; 26:1; Kum 28:38; 1 Fal 18:2; 2 Fal 8:1; Amu 17:8; Mik 5:2]
2Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrata wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko.[#Mwa 35:19; Amu 3:30; #1:2 maana yake ni ‘Mungu ni Mfalme’.; #1:2 maana yake ni ‘Mwema’.; #1:2 maana yake ni ‘Ugonjwa’.; #1:2 maana yake ni ‘Upotevu’.]
3Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili.
4Nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Baada ya kukakaa huko miaka kumi hivi,
5wote wawili Maloni na Kilioni wakafa; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia.
6Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana akiwa katika nchi ya Moabu alipata habari kuwa BWANA alikuwa amewajia watu wake na kuwapa chakula.[#Kut 4:31; Zab 80:14; Yer 29:10; Sef 2:7; Zek 10:3; Lk 1:68; 7:16; Mwa 28:20; 48:15; Kut 16:4,6; Zab 104:14,16; Mit 30:8; Isa 55:10; Mt 6:11]
7Basi akatoka pale alipokuwa akiishi, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda.
8Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia.[#Yos 24:15; 2 Tim 1:16]
9BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia.[#Rut 3:1]
10Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.
11Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, rudini; kwa nini mfuatane nami? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?[#Mwa 38:11; Kum 25:5]
12Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;
13je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu.[#Amu 2:15; Ayu 19:21; Zab 32:4; 38:2]
14Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye.[#Kum 4:4; 10:20; Mit 17:17; 18:24; Yn 6:66-69; Ebr 10:39]
15Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako.[#Yos 24:15-21; Amu 11:24]
16Naye Ruthu akasema,
Usinisihi nikuache,
Nirudi nisifuatane nawe;
Maana wewe uendako nitakwenda,
Na wewe ukaapo nitakaa.
Watu wako watakuwa watu wangu,
Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17Pale utakapofia ndipo nitakufa nami,[#1 Sam 3:17; 25:25; 2 Fal 6:31]
Na papo hapo nitazikwa;
BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi,
Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
18Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi.[#Mdo 21:14]
19Hivyo hao wakaendelea wote wawili hadi walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote uliwaajabia. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi?[#Mt 21:10; Isa 23:7; Omb 2:15]
20Akawaambia, Msiniite Naomi, niiteni Mara kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana.[#1:20 Tazama Rut 1:2.; #1:20 maana yake ni, ‘Uchungu’.]
21Mimi nilitoka nikiwa nimejaa, naye BWANA amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa BWANA ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?[#1 Sam 2:7,8; Ayu 1:21]
22Basi Naomi akarudi; pamoja na Ruthu Mmoabi, mkwewe; ambao walirudi kutoka nchi ya Moabu; nao wakafika Bethlehemu mwanzo wa mavuno ya shayiri.[#Kut 9:31; 2 Sam 21:9]