Yoshua Mwana wa Sira 11

Yoshua Mwana wa Sira 11

Uchangamfu wa Mwonekano

1Basi, hekima ya mnyonge itamwinulia kichwa chake, na kuketisha katikati ya wakuu.

2Usimsifu mtu kwa ajili ya uzuri wa uso, wala usimbeze kwa sababu ya sura yake.

3Nyuki ni mdogo katika warukao, bali matunda yake hupita tamutamu.

4Wala usione fahari juu ya mavazi yako, ukajikweza roho yako siku ya kuheshimiwa. Viumbe vyote vya BWANA vina ajabu, tena matendo yake yamefichwa na wanadamu;

5wafalme wengi wamekaa chini, naye yule asiyefikiriwa amevaa taji;

6mashujaa nao wamefedheheka, na watu mashuhuri wamesalitiwa.

Taamuli na Hadhari

7Usikaripie kabla hujachunguza;

Ufahamu kwanza, kisha ukemee.

8Usijibu kabla hujasikiliza;

Wala usijidukize kati ya usemi.

9Usilitetee jambo lisilo lako;

Wakosaji wakiamua usisimame.

10Mwanangu, mbona unazidi kujishughulisha na kazi nyingi? Afanyaye haraka kuongeza mali hataepuka hatia. Ukijihimiza kufuata utajiri hutapata, wala ukiutafuta hutauona.

11Kuna mtu ajitahidiye, na kufanya kazi, na kujihimiza; walakini kwa kadiri iyo hiyo huenda nyuma.

Kumtegemea Mungu peke yake

12Kuna aendaye polepole, na kuhitaji msaada, na kukosa nguvu, naye yu maskini kabisa; walakini macho ya BWANA yamemtazama kwa hisani, akampandisha kutoka unyonge wake,

13akamwinua kichwa chake na kumkweza, nao wengi wakastaajabu kwa kumwona.

14Mema na mabaya, uzima na mauti, umaskini na utajiri, hayo

15-16yote yatoka kwa BWANA.

17Ukarimu wa BWANA hukaa pamoja na mwenye haki, na hisani yake itamfanikisha daima.

18Kuna ajitajirishaye kwa werevu na kujinyima, na hii ndiyo sehemu ya thawabu yake;[#Zab 49:10; Lk 12:16-21]

19asemapo, Nimeona raha na sasa nitakula mapato yangu, yeye hajui baada ya siku ngapi atawapisha wengine na kufa.

20Usimame thabiti katika agano lako, ujizoeze nalo, ili udumu katika kazi yako hata uzeeni.

21Usisituke kwa kuona matendo ya mkosefu, bali umtumaini BWANA, na kudumu katika kazi yako; kwa maana ni vyepesi machoni pa BWANA ghafla kumfanya maskini kuwa tajiri.

22Baraka ya BWANA ni thawabu ya mwenye akili, na katika saa moja ijayo upesi huisitawisha baraka yake.

23Usiseme, Ninafaa nini, na tangu sasa mema yangu yatatoka wapi?

24Usiseme, Nimetoshewa, na tangu sasa mabaya gani yawezayo kunitukia?

25Siku ya mema mabaya husahauliwa, vile vile siku ya mabaya mtu hakumbuki mema.

26Ni vyepesi machoni pa BWANA kumjazi mtu siku ya kufa kwake sawasawa na mwenendo wake.

27Tena taabu ya saa moja huleta usahaulifu wa furaha; na mwisho wa mtu ndio ulio ufunuo wa habari zake.

28Usimwite mtu heri kabla ya kufa kwake; aidha, mtu hujulikana kwa kuwatazama watoto wake.

Uangalifu katika Kuchagua Marafiki

29Usimwingize kila mtu nyumbani mwako; kwa maana msingiziaji anayo mashauri mengi.

30Kama kware wa mwindaji katika tundu, ndivyo ulivyo moyo wa mwenye kiburi; na mfano wa mpelelezi atakutazamia kuanguka kwako.

31Maana yake huotea ili kugeuza mema kuwa mabaya, na yale yastahiliyo kusifiwa atayalaumu.

32Cheche ya moto huwasha chungu nzima ya makaa; na mtu wa dhambi kuvizia damu.

33Ujihadhari na mtu mwovu, ambaye hutunga maovu; asije akaleta lawama juu yako hata milele.

34Ukimpokea aliye mgeni nyumbani mwako, atakutia wasiwasi kwa makelele yake, hata kukufarikisha nao walio wako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya