Yoshua Mwana wa Sira 16

Yoshua Mwana wa Sira 16

Adhabu ya Mungu kwa wenye Dhambi

1Usitamani kuwa na watoto wengi wasiofaa, wala usiwafurahie wana wasiomcha Mungu.

2Hata wakizaa usiwafurahie, isipokuwa ni watu wamchao BWANA.

3Usitumainie uhai wao, wala usiutegemee mwisho wao, ambao hawatapata kufa kwema; kwa maana ni afadhali mmoja mcha Mungu kuliko elfu wakosaji, ni afadhali kufa huna wana kuliko kuwa na watoto wasiomcha Mungu.

4Kutoka kwa mtu mmoja mcha Mungu asiye na mwana mji utakuja kukaliwa na watu, bali taifa zima la watu wabaya watafanyika ukiwa.

5Mambo mengi ya namna hiyo nimeyaona kwa macho yangu, tena kwa sikio langu nimesikia mambo makuu kuliko hayo.

6Katika kusanyiko la wenye dhambi moto utawashwa, na katika taifa asi ghadhabu huwaka.

7BWANA hakuwaridhia wakuu wa kale walioasi katika nguvu zao;[#Hek 14:6]

8Yeye hakuwaachilia wale ambao Lutu alikaa kwao, wale aliowakirihi kwa kiburi chao;

9hakuwahurumia watu wa upotevu walioondolewa katika dhambi zao;

10vile vile watu wale elfu mia sita walioangamia katika ugumu wa mioyo yao,

11hata akiwapo mtu mmoja mwenye shingo ngumu, ni ajabu akiepukana na adhabu yake. Kwa maana rehema na ghadhabu zina yeye, naye yu hodari wa kusamehe, pia na humwaga ghadhabu juu ya waovu.

12Kama zilivyo kuu rehema zake, ndivyo ilivyo na adhabu yake; humhukumu mtu sawasawa na matendo yake.

13Mwenye dhambi hataokoka na mapato yake, wala tumaini la mwenye haki halitabatilika.

14Kwa kila kazi ya rehema atafanya nafasi, na kila mtu ataona thawabu sawasawa na matendo yake.

Malipo na Hakika

17Lakini usiseme hivi, Mimi nitafichwa na BWANA, naye yu nani atakayenikumbuka mimi kutoka juu? Mimi sitambulikani katikati ya watu wengi, kwa maana roho yangu moja ni kitu gani miongoni mwa viumbe visivyo na idadi?

18Tazama, mbingu, na mbingu za mbingu, na vilindi, na dunia, na vyote vilivyomo, vitatikisika atakapokuja Yeye;

19milima, hata na misingi ya nchi, inatetemeshwa aitazamapo Yeye.

20Yakini hakunitia mimi moyoni mwake, naye yu nani mwenye kuzichungulia njia zangu mimi?

21Nikitenda dhambi hakuna jicho la kuiona, na kama nikafanya hila kwa siri yu nani ajuaye?

22Pia ni nani mwenye kuyasimulia matendo yangu ya haki, tena tumaini lipi, maadamu hukumu iko mbali?

23Ndivyo afikirivyo mtu asiye na ufahamu na mpumbavu desturi yake huwaza mapumbavu.

Busara ya Mungu Yaonekana katika Uumbaji

24Mwanangu, unisikilize na kuipokea hekima yangu, na kuyaangalia maneno yangu moyoni mwako.

25Mimi nitatoa mafundisho kwa kipimo, na kutangaza maarifa kwa uangalifu.

26Hapo mwanzo Mungu alipoiumba kazi yake, na tangu alipoifanya, aliamuru aina zake.

27Aliviratibisha viumbe vyake milele,

Na mianzo yake hata vizazi vyote.

Havioni njaa, wala havichoki,

Wala havikomi hatika kazi zake.

28Hakuna chenye kusukuma jirani yake,

Wala haviasi neno lake kamwe.

29Baada ya hayo tena BWANA aliitazama nchi, akaijaza mibaraka yake.

30Kwa kila namna ya viumbe vyenye uhai akaufunika uso wake, na ndani yake vinarudi vyote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya