The chat will start when you send the first message.
1BWANA alimuumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha.[#Mwa 1:26-28; 2:7]
2Akawapa wanadamu siku kwa idadi, na muhula iliyoamriwa; akawapa amri juu ya vitu vilivyomo;
3akawavika nguvu kama Yeye mwenyewe, na kuwafanya kwa mfano wake.
4Akaitia hofu ya binadamu katika vyote vyenye mwili,
5ili wawatawale wanyama na ndege.
6Akawajaza maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu.
7Akawafanyizia ulimi, na macho, na masikio akawapa na moyo wa ufahamu.[#Mwa 2:17]
8Ili kuwaonesha adhama ya kazi yake,
9Ili wasijisifie katika miujiza yake,
10Na kukijulisha kicho chake ulimwenguni,
Na kulihimidi jina lake takatifu;
11Aliyaweka mbele yao maarifa,
Akawapa sheria ya uzima kuwa urithi.
12Alifanya nao wateule wake agano la milele, na kuwaonesha hukumu zake.
13Kwa macho yao waliiona enzi ya utukufu wake, na kwa masikio yao waliisikia sauti yake yenye nguvu.
14Akawaambia, Jihadharini na yasiyo haki, akawapa amri kila mtu juu ya jirani yake.
15Njia zao nazo zi mbele zake daima,
16wala hazitafichwa machoni pake.
17Kwa kila taifa aliamuru mfalme,
18Bali Israeli ni kura yake BWANA.
19Matendo yao ni kama jua mbele zake,
Na mawazo yao ni dhahiri kwake.
20Kwake makosa yao hayakufichika,
21Na dhambi zao zote zipo mbele zake.
22Lakini kwake Yeye sadaka za mtu ni kama pete ya mhuri, naye ataweka akiba ukarimu wa wanadamu kama mboni ya jicho;
23hatimaye atatokea na kuwapa thawabu, naye atawalipa waovu uovu wao juu ya vichwa vyao.
24Hata hivyo huwajalia wale watubuo kurudi, na wao wanaopotewa na saburi huwafariji.
25Basi umrudie BWANA na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo;[#Yer 3:12]
26umgeukie tena Yeye Aliye Juu, uyageuze maovu, uyakirihi yaliyo machukizo.
27Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani.[#Zab 6:5; Isa 38:18; Bar 2:17-18]
28Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi BWANA.
29Ee ajabu ya wingi wa rehema za BWANA, na ya masamaha yake kwao wanaomgeukia!
30Sivyo ilivyo kwa wanadamu,
Wala wazo lake si mawazo yao.
31Nini ing'aayo kuliko jua? Ila lafifia;
Kadhalika yule asiyezuia tamaa.
32Mungu huwahukumu majeshi ya mbinguni,
Na wanadamu wote ni mavumbi na majivu.