Yoshua Mwana wa Sira 19

Yoshua Mwana wa Sira 19

1Afanyaye hivyo hapati kuwa tajiri; wala kibarua aliye mlevi!

Anayedharau mambo madogo

Ataanguka kidogo kidogo.

2Vileo na wanawake huwaangamiza hata watu wa ufahamu, na yule awaendeaye makahaba ataharibika;

3nondo na funza watamrithi, na roho ya mfidhuli ni harabu ya mwenyewe.

Kuhusu Mazungumzo Yasiyofaa

4Mfanya haraka kutawakali hana ufahamu, naye mtenda dhambi hukosa juu ya roho yake mwenyewe.

5Mwenye kuchangamka katika uovu rohoni mwake atahukumiwa;

6lakini mtu asiyependa udakuzi anao uovu uliopungua.

7Basi yale uliyoambiwa usinene tena kamwe; hutazidi kuwa na hali mbaya.

8Na iwe habari ya rafiki au adui, usinene; isipokuwa ni dhambi kwako usiifunue;

9asije yule akasikia, na kukuchunguza, na wakati utakapowadia atakuchukia.

10Je! Wewe umesikia neno? Na life pamoja nawe; jipe moyo mkuu, halitakupasua.

11Bali mpumbavu atakuwa na uchungu wa neno kama vile mwanamke aonavyo uchungu wa kuzaa mwana;

12tena kama mshale uchomao nyama ya pajani, ndivyo ilivyo neno tumboni mwa mpumbavu.

Uhakikishe kwanza mambo Unayosikia

13Mhoji rafiki yako; labda hakulitenda, hata iwapo amelitenda yawezekana asizidi kulitenda.

14Mhoji jirani yako; labda hakulisema, hata iwapo amelisema yawezekana asiliseme tena.

15Basi mhoji rafiki yako; mara nyingi huwa visingizio tu, wala usiliamini kila neno.

16Aidha, kuna atelezaye kwa ulimi, wala si kwa moyo; kwa maana ni nani asiyekosa kwa ulimi wake?

17-18-19Basi mhoji jirani yako kabla ya kumtisha, uipishe torati yake Aliye Juu.

Hekima ya kweli na ya Uongo

20Hekima yote ni kumcha BWANA;

21na katika hekima yote mna kutenda kwa torati;

22wala kujua maovu siyo hekima; wala shauri la wenye dhambi siyo busara.

23Tena kuna werevu, ambao ni chukizo; tena kuna ujinga, ambao ni upungufu wa akili;

24yule aliye na ufahamu kidogo tu pamoja na kicho humpita mtu aliye mwingi wa busara bali anaivunja torati.

25Yuko mwerevu halisi wala hana haki; yuko tena mtu mwenye staha ya hila ili apate hukumu.

26Pia yuko atendaye mabaya sana, huinama kichwa kwa huzuni, bali ndani amejaa hila;

27hukunja uso, hufanya kana kwamba yu kiziwi katika sikio moja; naye pale pale asipojulikana atakughilibu.

28Na ikiwa kwa kukosa uwezo amezuiwa asitende dhambi, mara apatapo nafasi atafanya madhara.

29Kila mtu atatambulikana kwa uso wake; mwenye ufahamu atajulikana kwa sura yake popote umkutapo;

30nazo nguo za mtu, na cheko la kutoa meno, na mwendo wake, huonesha mara alivyo yeye mwenyewe.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya