Yoshua Mwana wa Sira 25

Yoshua Mwana wa Sira 25

Wastahilio Sifa

1Kuna mambo matatu yanipendezayo,

Ni mazuri mbele za Mungu na wanadamu;

Umoja wa ndugu,

Urafiki wa majirani,

Na mke na mumewe wanaopatana.

2Kuna watu wa namna tatu wanichukizao,

Na mwenendo wao unanikirihi;

Maskini mwenye kiburi,

Tajiri aliye mwongo,

Na mzee mzinifu asiye na ufahamu.

Wazee

3Katika ujana wako hukukusanya

Utapata wapi upatapo kuwa mzee?

4Ee ajabu ya uzuri wa uteuzi kwao wenye mvi, na kwa wakuu wajuao shauri!

5Ni nzuri kama nini hekima ya wazee, na mawazo yenye shauri ya wale walioheshimiwa!

6Ustadi wa kuzoea ni taji la wazee, na utukufu wao ni kumcha BWANA.

Mithali ya hesabu

7Kuna mambo tisa niliyoyafikiri,

Na moyoni mwangu nimeyaita heri;

Mtu mwenye kuwafurahia watoto wake,

Aliye hai akaona adui zake wamepotea,

8Heri yule mume mwenye mke wa ufahamu.

Naye yule asiyeteleza kwa ulimi wake.

Naye asiyemtumikia mtu asiyestahili,

9Naye yu heri aliyejipatia rafiki amini,

Naye asemaye masikioni mwa wasikivu,

10Naye aipataye hekima ni mkuu kama nini!

Lakini hakuna ampitaye mcha BWANA.

11Hakika kicho cha BWANA hupita mambo yote;

12Aliye nacho aweza kulinganishwa na nani?

Baadhi ya Uovu Uliokithiri

13Msiba wowote ila msiba wa moyo;

Uovu wowote ila uovu wa mwanamke;

14Baa lolote ila litokalo wanichukiao;

Kisasi chochote ila kisasi cha adui;

15Hakuna sumu ipitayo sumu ya nyoka;

Hakuna hasira kuliko hasira ya mtesi.

Uovu wa Mwanamke Mbaya

16Ningependa kukaa na simba na joka kuliko kukaa nyumbani pamoja na mwanamke mbaya,

17Ubaya wa mwanamke huubadili uso wake kuwa wa kutisha, na kumtia sura yake giza kama ya dubu.

18Mumewe akikaa chakulani pamoja na jirani zake, bila kusudi aweza kupiga kite kwa majonzi.

19Ukorofi wote si kitu kama ukorofi wa mwanamke; mwenye dhambi na ampate kuwa sehemu yake!

20Kama kuipanda njia ya mchangani kwa miguu ya mzee, ndivyo alivyo mke mwenye maneno mengi kwa mtu mtulivu.

21Usinaswe na uzuri wa mwanamke, wala usimtamani mwanamke kwa ajili ya mali yake.

22Kuna utumwa mzito, na fedheha, iwapo mwanamke humlisha mumewe.

23Mwanamke mbaya ni unyong'onyevu wa roho, na huzuni ya uso, na kujeruhi moyoni. Mwanamke asiyetaka kumfurahisha mumewe amefanana na mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza.

24Mwanzo wa dhambi ulitoka katika mwanamke, na kwa sababu yake sisi sote tunakufa.

25Usiyapatie maji mahali pa kutoka, wala usimpe mwanamke mbaya nafasi ya kusema kwa ujasiri.

26Tena iwapo haendi kama wewe utakavyo, mpe hati ya talaka.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya