The chat will start when you send the first message.
1Mwenye kurehemu atamkopesha jirani yake; naye mwenye kumnafisisha mwenzake huzishika amri.[#Kut 22:25; Law 25:35-38]
2Umkopeshe jirani yako alipo ana haja; pia umlipe jirani yako wakati ukiwadia.
3Thibitisha neno lako, na uwe mwaminifu kwake; nawe utapata mahitaji yako kila wakati.
4Kuna wengi waliouona ukopi kuwa ni pato la bahati, wakawasumbua sana waliowasaidia.
5Hata apokee, huyo atabusu mikono, na kuinyenyekeza kauli yake, kwa ajili ya fedha za mwenzake; la! Wakati wa kulipa ataongeza siku, na kusikitika, na kulalamikia majira.
6Yule akidiriki, atapata nusu tu kwa shida, ataihesabia ni bahati yake; la! Sivyo, amenyimwa fedha zake, pia na kupata adui bure. Naye huyo, kulipa atalipa kwa laana na ufidhuli, atamrudishia mzaha badala ya heshima.
7Hivyo wengi wamegeuka upande, si kwa sababu ya ubahili, ila hawataki kuhadaiwa bure.
8Walakini kwa habari ya mtu maskini uwe mvumilivu, na kumwongezea siku kwa huruma.
9Umsaidie maskini kwa ajili ya amri; na kadiri ulivyo ukata wake usimfukuze mikono mitupu.
10Poteza fedha zako kwa ajili ya ndugu yako na rafiki yako, zisiharibike kwa kutu chini ya jiwe.
11Toa hazina yako sawasawa na amri zake Aliye Juu, itakufaidia kuliko dhahabu.
12Ujiwekee sadaka katika hazina yako, itakuokoa katika kila taabu;
13itakupigania juu ya yule adui kuliko ngao kubwa na mkuki wenye nguvu.
14Mtu aliye mwema atamdhamini mwenzake; wala huyo hatamkimbia isipokuwa amepotewa na haya.
15Wala usisahau fadhili zake mdhamini wako, ambaye amekutolea maisha yake.
16Mkosefu aweza kuiharibu hali njema ya mdhamini wake, na mwenye nia mbovu atamfilisisha yeye aliyemwokoa.
17Kweli udhamini umewapoteza wengi waliofanikiwa, na kuwatikisa kama wimbi la bahari;
18naam, kuna matajiri waliofukuzwa nyumbani, na kutangatanga katika nchi za kigeni.
19Basi, mkosaji akitumbukia udhamini kwa kutodiriki mikataba ya kazi, ataanguka hukumuni.
20Hivyo, umsaidie jirani yako kadiri uwezavyo, lakini ujiangalie nafsi yako usije ukaangamia.
21Katika maisha ya mwanadamu neno kubwa ni maji, na chakula, nguo, na nyumba ya kujifichia humo.
22Afadhali maisha ya maskini katika kibanda cha miti, kuliko kula anasa katika nyumba ya mwingine.
23Kwamba una kidogo au kwamba una wingi uwe radhi, maana ni maisha ya taabu kwenda toka nyumba hata nyumba;
24ukaapo, nawe u mgeni, wewe hutathubutu kufumbua kinywa chako.
25Utaandaa meza, na kupitisha vileo, na kukosa shukrani; pamoja na hayo utasikia maneno mengi ya uchungu.
26Njoo hapa, mgeni,
Andaa meza;
Una kitu mkononi?
Nilishe nacho.
27Ondoka, mgeni,
Kutoka kwa heshima;
Ndugu yangu amekuja;
Nataka nyumba yangu.
28Haya ni magumu kwa mwenye ufahamu;
Makaripio, na riba, na ukopi.