The chat will start when you send the first message.
1Kuzilinda mali kwadhoofisha mwili, na kuzisumbukia kwaondoa usingizi.
2Pia kuzisumbukia riziki hufukuza usingizi zaidi ya ugonjwa mbaya unaomzuia mtu asilale unono.
3Mtu aliye tajiri hufanya kazi katika kukusanya mali, naye anapopumzika amejaa anasa zake;
4mtu aliye maskini hufanya kazi katika upungufu wa riziki, na yeye anapopumzika ameingia uhitaji.
5Mpenda dhahabu hatahakikishwa, naye aifuataye faida atapoteza njia.
6Watu wengi wameangamia kwa ajili ya dhahabu, na upotevu wao utawakuta uso kwa uso.
7Ndiyo kikwazo kwa wale wanaoitamani, na kila mpumbavu atanaswa nayo.
8Yu heri tajiri aliyeonekana hana ila,
Hakuifuata dhahabu wala kuitamani fedha.
9Ni nani huyu?
Nasi tutamwita heri;
Ametenda mambo ya ajabu kati ya watu.
10Nani aliyejaribiwa,
Akaonekana amekamilika?
Ajisifie hasa maisha ya amani maridhawa.
Nani aliyeweza kuasi,
Wala yeye hakuasi?
Aliyeweza kutenda mabaya.
Wala yeye hakuyatenda?
11Mapato yake yatathibitishwa kwake;
Na kusanyiko watangaza sadaka zake.
12Mwanangu, ikiwa umeketi mezani pa mkuu, usiwe na choyo pale pale, wala usiseme, Aha! Vyakula vingi hapa.
13Fikiri ya kuwa kijicho ni uovu. Hakuna kitu kilichoumbwa kibaya kuliko jicho, kwa hiyo latoka machozi kwa kila sababu.
14Usiunyoshe mkono wako kila utazamapo, wala kujisongeza pamoja nao kwenye sahani.
15Fikiri apendavyo jirani yako, na kwa vitu vile usivyopenda tumia busara.
16Kula vitu vile vilivyowekwa mbele yako kama impasavyo mtu mzima, ila usile kwa pupa usije ukachukiwa.
17Uwe wa kwanza wa kuacha kula, kwa ajili ya adabu, tena usiwe mlafi usije ukachukiza.
18Na iwapo unakula pamoja na wengi, usiunyoshe mkono wako mbele ya jirani yako.
19Mtu mwenye adabu aweza kushiba kwa chakula kidogo tu, wala hatapiki kitandani pake.
20Maumivu na kukosa usingizi, na msokoto, na tumbo, humpata asiyetosheleka. Usingizi wenye afya hutoka katika kula kwa kiasi; mtu huondoka mapema na akili zake anazo.
21Iwapo umeshawishika kula sana, uondoke katikati nawe utapata raha.
22Mwanangu, unisikilize, usinidharau, mwishowe utaona maneno yangu ni kweli. Katika matendo yako yote uwe na kiasi, dhara lisikujie.
23Aliye mkarimu wa chakula midomo itamsifu,
Na ushuhuda wa wema wake utathibitika;
24Aliye bahili wa chakula mji utamzomea,
Na ushuhuda wa ubahili wake utathibitika.
25Usijioneshe kuwa hodari wa kunywa kileo, yaani, mvinyo imewaangamiza wengi.
26Tanuri hujaribu kazi ya mhunzi, na mvinyo mioyo ya watu, katika ugomvi wa wenye kiburi.
27Kwa wanadamu mvinyo ni kama maji ya uzima, ukinywa kwa kiasi; je! Anao uzima gani mtu asiye na mvinyo? Nayo imeumbwa ili kuwafurahisha wanadamu.
28Mvinyo ni furaha ya moyo na changamko ya roho, ikinywewa kwa wakati wake na ya kutosha.
29Lakini kunywa mno ni uchungu wa roho, na fedheha, na ugomvi.
30Kileo humzidishia mpumbavu mitego ya kumletea hasara; hupunguza nguvu, na zaidi huleta jeraha.
31Usimkaripie jirani yako penye karamu ya mvinyo, wala usimdhihaki anapocheka; wala usimwambie neno la shutumu, wala usimsumbue kwa kutaka alipe deni.