The chat will start when you send the first message.
1Umheshimu tabibu kwa kadiri ulivyo na haja naye, na kwa heshima iliyo haki yake, kwa kuwa BWANA amemwinua kweli kweli.
2Kwa maana ni kutoka kwake Aliye Juu tabibu alivyoupata ufundi wake, hata na kwa mfalme atapokea ada.
3Maarifa yake tabibu yatamwinua kichwa chake, naye atasimama ni mkuu machoni pa wakuu.
4BWANA ameyaotesha madawa katika nchi, wala mwenye busara hatayadharau.
5Je! Maji hayakutiwa utamu kwa mti, ili Mungu awaonyshe watu wote uweza wake?[#Kut 15:23-25]
6Naye amewapa wanadamu maarifa, ili atukuzwe mwenyewe kwa ajili ya miujiza yake.
7Kwa hayo mponya watu huwatulizia wote maumivu yao; kwa hayo mfanyiza dawa huyafanya machanganyiko yake;
8ili isikome kazi ya Mungu, wala siha njema isibatilike katikati ya wanadamu.
9Basi, mwanangu, ugonjwani usiwe mfidhuli; lakini umwombe Mungu na Yeye atakuponya.
10Ujitenge na dhambi, na kujitengeneza moyo, na kujisafisha mikono na kila namna ya uovu.
11Toa sadaka ya unga, na kumbukumbu, na dhabihu ya vinono, kwa kadiri ya mali ulizo nazo.
12Kisha mpishe tabibu, wala asiondoke kwako, kwa maana una haja naye.
13Kwa kuwa pengine kuna muda na hali njema imo hasa mikononi mwao.
14Maana hao nao humsihi BWANA, kwamba awafanikishe katika kuuyakinisha ugonjwa, na kuwapatia watu nafuu, na kuuhifadhi uhai wenyewe.
15Na mtu yeyote atendaye dhambi mbele za Mola wake, ni afadhali sana aanguke katika mikono ya tabibu.
16Mwanangu, machozi yako yadondoke juu yake aliyefariki, na katika uchungu wa roho yako ufanye maombolezo; umfunge sanda mwili wake kama ilivyo haki yake, wala usijifiche wakati wa kumzika.[#Sira 22:11-12]
17Fanya kilio kwa huzuni, na maombolezo makuu; na matanga yake yawe sawasawa na stahili zake, siku moja au mbili, usije ukaona fedheha; hivyo uburudike moyo wako katika huzuni yako.
18Kwa maana huzuni izidiyo huleta mauti, na uchungu wa rohoni hula nguvu.
19Atakapochukuliwa maiti ni afadhali huzuni ipite, mradi maisha ya kusikitika yaweza kuudhuru moyo.
20Usiweke huzuni moyoni mwako, uiweke mbali nawe ukiukumbuka mwisho wako;
21usisahau ya kwamba hakuna kurudi tena; hutamfaidia yeye, nawe utajidhuru mwenyewe.
22Uikumbuke amri iliyo juu yake, nayo ni juu yako pia; jana kwake na kesho kwako.
23Basi atakapostarehe yeye aliyefariki, na ukae ukumbusho wake; roho yake ikiisha kuondoka, ujiburudishe moyo wako kwa ajili yake.
24Hekima ya mwandishi hurejea wasaa wa faragha, naye mwenye shughuli haba ndiye atakayepata hekima.
25Bali ataipata wapi mtu yule ashikaye plau, na kuona fahari juu ya mti wa mchokoo, na kuswaga ng'ombe, na kujishughulisha nao, na kuzungumza nasaba ya mafahali?
26Huyo atautia moyo wake katika kuifudikiza mifuo yake, na nadhari yake ni kuwapa ndama zake malisho.
27Ndivyo alivyo kila aliye msanii mwenye ufundi, ashikaye kazi usiku na mchana. Anayechora nakshi ya mhuri hufanya bidii ya kutofautisha namna nyingi mbalimbali; na kuutia moyo wake katika kuuhifadhi ulingano akichora sanamu, na hadhari yake ni kuimaliza kazi yake.
28Mhunzi naye hukaa penye fuawe, na kuifikiri sana chuma kitupu; ufukuto wa moto utatokeza malengelenge, naye atashindana na joto la tanuri; sauti ya nyundo itamfanya kiziwi, na macho yake ameyakaza juu ya umbo la chombo. Huyo atautia moyo wake katika kuikamilisha kazi yake, na hadhari yake ni kuipamba kwa ustadi.
29Na mfinyanzi naye ni vile vile, huketi kazini, na kuizungusha gurudumu kwa miguu; sikuzote huisumbukia kazi yake, kwa kuwa maishilio yake yote ni kwa jumla ya vyombo vyake;
30huumba udongo kwa mikono yake, na kuukanda mbele ya miguu yake. Huyo atautia moyo wake katika kumaliza kupaka rangi, na hadhari yake ni kusafisha joko.
31Hao wote huitegemea mikono yao, na kila mmoja huchuma ufundi wa kazi yake.
32Pasipo hao mji hauwezi kukaliwa na watu, wala hao hawatakosa riziki wakaapo pote.
33Kweli hao hawatatafutwa katika mkutano wa wakuu, wala katika baraza hawatapanda juu, wala kuketi katika kiti cha hakimu, wala kuelewa na agano la hukumu.
34Hata na elimu na maagizo ya hekima hawatayatangaza, wala kuonekana miongoni mwao wasemao kwa mithali. Bali hata hivyo ndio hao wanaodumisha maumbile ya ulimwengu, na kazi yao stadi ndiyo sala yao.