The chat will start when you send the first message.
1Yoshua mwana wa Nuni alikuwa mtu hodari wa vita, na mtumishi wa Musa katika kazi ya unabii. Kama lilivyokuwa jina lake akakuzwa, awe wokovu mkuu wa wateule wa Mungu; ili kuwalipiza kisasi adui waliowaondokea; ili kuwapa Israeli urithi wao.[#Yos 1:1—11:23]
2Jinsi alivyokuzwa akinyosha mkono wake,
Alipoufuta upanga wake juu ya mji!
3Ni nani aliyeweza kusimama mbele yake,
Mradi alipigana vita vya BWANA?
4Je! Jua halikusimama kwa amri yake,
Hata siku moja ikawa kama mbili?
5Kwa maana alimwita Mungu Aliye Juu,
Adui zake walipomsonga pande zote.
Naye Mungu Aliye Juu akamwitikia kwa mvua ya mawe ya barafu;
6Yeye akayatupa kwa nguvu juu ya taifa la adui; na penye yale materemko akawaangamiza wale walioipinga njia; ili mataifa yote waliolaaniwa wapate kujua ya kwamba BWANA alikuwa akichungulia kupigana kwao.
7Na ya kuwa huyo alimfuata Mungu kwa moyo wake wote. Tena siku za Musa huyo alifanya kazi ya utauwa, yeye pamoja na Kalebu mwana wa Yefune, kwa vile walivyosimama imara mkutano walipotupa kiasi, ili kugeuzia hasira mbali na makusanyiko, na kuyatuliza manung'uniko ya uovu.[#Hes 14:6-10; 11:21; Yos 14:6-11]
8Basi katika watu elfu mia sita hao wawili wakahifadhika peke yao, ili kuwaleta katika urithi wao, katika nchi iliyojaa maziwa na asali.
9Na Kalebu naye BWANA akamjalia nguvu, ikakaa naye hata uzee wake, apakanyage mahali pa nchi palipoinuka, na wazao wake wakapapate kuwa urithi;
10ndiyo maana wazao wa Yakobo wajue ya kwamba ni kuzuri kumfuata BWANA.
11Pia na waamuzi, kila mmoja kwa jina lake, wote ambao mioyo yao haikudanganywa, wala hawakugeukia mbali na BWANA, kumbukumbu lao na libarikiwe.[#Amu 1:1—16:31]
12Hata na mifupa yao ifanikiwe panapo makao yao, na majina ya hao wenye kuheshimiwa yachipuke miongoni mwa watoto wao.
13Samweli aliheshimiwa na watu wake, akapendwa na Mola wake, ambaye akaazimwa kwa BWANA toka tumboni mwa mamaye; mnadhiri wa BWANA katika unabii, mwamuzi na mfanya kazi ya ukuhani. Yeye kwa neno la Mungu aliuratibisha ufalme, na kuwapaka mafuta watawala wa watu wake.[#1 Sam 3:19-20; 7:9-11; 10:1; 12:3; 16:13; 28:18-19]
14Kwa Torati ya BWANA aliwaamua watu,
Naye BWANA akawajilia Yakobo.
15Kwa uaminifu akawa mwona aulizwaye,
Na kwa jibu lake akawa mwona amini.
16Adui walipomsonga alimwita Aliye hodari,
Akitoa dhabihu ya mwana-kondoo;
17BWANA naye akanguruma kutoka mbinguni,
Na kwa mshindo akaisikiza sauti yake.
18Yeye naye aliwaangamiza kabisa wakuu wa maadui, na mabwana wote wa Wafilisti.
19Na wakati alipokuwa tayari kulala usingizi wa mauti, mbele za BWANA na mbele ya Masihi wake alijitetea kwa ujasiri, Kwa mkono wa nani nimepokea rushwa, hata jozi ya viatu? Wala hakuna aliyemshitaki.
20Hata akiisha kufariki aliulizwa unabii, akamjulisha mfalme mwisho wake, akaiinua sauti yake kutoa unabii kutoka chini ya nchi, ili kuufuta uovu wa watu.