Yoshua Mwana wa Sira 47

Yoshua Mwana wa Sira 47

Nathani

1Baada yake akasimama Nathani ili atoe unabii zamani za Daudi.[#2 Sam 7:2-3; 12:1]

Daudi

2Kama mafuta yalivyotengwa na kafara ya amani, vivyo hivyo Daudi alitengwa na wana wa Israeli.[#1 Sam 17:34—18:7; 2 Sam 5:7; 8:1; 12:13]

3Naye alicheza pamoja na simba kana kwamba ni wana-mbuzi, pia pamoja na dubu kana kwamba ni wana-kondoo wa kundi.

4Je! Hakumwua jitu katika ujana wake,

Akawaondolea watu lawama;

Alipouinua mkono wake na jiwe la teo,

Akayashusha majivuno ya Goliathi?

5Kwa maana alimwita Aliye Juu;

Na yeye akaitia nguvu yamini yake;

Ili amwue shujaa hodari wa vita;

Ili aiinue pembe ya watu wake.

6Kwa hiyo binti za watu wakamtukuza wakiimbiana, na kumheshimu alivyoua makumi elfu yake; naye alipokwisha kuivaa taji la utukufu,

7alipigana na adui na kuwashinda pande zote; akajenga maboma yake kati ya Wafilisti, akaivunja pembe yao vipande vipande, hata siku hii ya leo.

8Katika kila kazi yake Daudi alimshukuru Mungu Aliye Juu kwa maneno matukufu; na kwa moyo wake wote akampenda Mola wake, akamhimidi kila siku daima.

9Pia akaweka waimbaji mbele ya madhabahu, ili watoe sauti tamu katika kuimba kwao.

10Akauongeza uzuri wa sikukuu, akaziratibisha nyakati katika ukamilifu; pindi walipolihimidi jina takatifu la BWANA, hata patakatifu pakavuma sauti tokea asubuhi na mapema.

11Naye BWANA akamwondolea dhambi zake, akiinua pembe yake hata milele; akampa agano la ufalme, na kiti kitakatifu cha enzi katika Israeli.

Sulemani

12Na kwa ajili yake akainuliwa mwanawe, mtu wa ufahamu aliyekaa salama.

13Sulemani alimiliki katika siku za kufanikiwa; naye Mungu akampa raha kumzunguka pande zote; ili alijengee jina lake nyumba, na kumwekea tayari patakatifu pa milele.[#1 Fal 4:21-32]

14Jinsi ulivyohekimishwa ujanani,

Na kujazwa ufahamu kama Nile!

15Nafsi yako uliifunikiza nchi,

Na kuikusanya mifano kama bahari.

16Jina lako likafikia visiwa vya mbali,

Nao wakaisikilizia habari yako;

17Kwa nyimbo, na mithali, na tafsiri,

Ukawastaajabisha watu wote.

18Katika jina la BWANA Mungu,[#1 Fal 10:21,27]

Aitwaye Mungu wa Israeli,

Ulikusanya dhahabu kama chuma,

Na kuzidisha fedha kama mawe.

19Ila kwa wanawake uliinamisha viuno,[#1 Fal 11:1]

Na kutiishwa mwili wako;

20Hivyo uliitupa heshima yako,

Na kukinajisi kitanda chako.

Uliwaletea wanao ghadhabu;

Kuna sikitiko kwa upuzi wako;

21Hata ufalme ukagawanyika,[#1 Fal 12:15-20]

Wakatawala waasi katika Efraimu.

22Bali BWANA hataiacha rehema yake,[#1 Sam 7:15]

Wala kulivunja neno lake;

Hatawafuta wazao wa mteule wake,

Wala kuharibu uzao wa mpenzi wake.

Basi, akamjalia Yakobo mabaki, na Daudi shina limtokalo.

Rehoboamu na Yeroboamu

23Naye Sulemani akastarehe pamoja na baba zake. Huyo ndiye aliyemwacha nyuma yake, katika wazao wake, Rehoboamu, mpumbavu kabisa, asiyekuwa na ufahamu hata kidogo; ambaye aliwachukiza watu kwa shauri lake hata wakaasi.[#1 Fal 11:43; 12:10-30; 2 Fal 17:6,18]

Yeroboamu

24Yeroboamu mwana wa Nebati naye, aliyewakosesha Israeli, akawapatia Waefraimu kikwazo, hata wafukuzwe katika nchi yao. Tena dhambi zao zikaongezeka mno ajabu;

25mradi walijiuza kutenda kila namna ya uovu, hata kisasi kiwaangukie.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya