The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, aliposimama Nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuri.[#1 Fal 17:1-24; 18:38; 19:15-16; 2 Fal 1:10-16; Mal 4:5-6]
2Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao;
3kwa neno la BWANA akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akateremsha moto.
4Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako!
Aliye mfano wako ataona fahari.
5Aliyekufa ulimfufua katika mauti,
Kutoka kuzimu, kwa neno la BWANA.
6Ukawashusha wafalme mpaka shimoni,
Na watu wateule vitandani mwao.
7Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi,
Na nabii ili akufuate nyuma yako.
8Ulisikia makaripio huko Sinai,
Na hukumu za kisasi huko Horebu.
9Ukachukuliwa juu katika kisulisuli,
Katika gari la farasi wa moto.
10Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo,
Ili kutuliza hasira siku ile ya BWANA;
Kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana
Na kuhuisha kabila za Israeli.
11Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.
12Ndiye huyo Eliya aliyefunikwa kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote.[#2 Fal 2:9,13]
13Hakukutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii;[#2 Fal 13:20-21]
14kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na katika mauti yake kazi zake zikawa za ajabu.
15Lakini kwa ajili ya hayo yote watu hawakutubu, wala hawakuziacha dhambi zao; hata walipochukuliwa mateka kutoka nchi yao, wakatawanyika juu ya uso wa dunia yote.[#2 Fal 18:11-12]
16Kisha walisalia katika Yuda watu wachache sana, ila mtawala akabaki katika mbari ya Daudi. Na baadhi yao wakatenda maadili, na baadhi yao wakazidi kutenda dhambi.
17Hezekia aliujengea mji wake maboma, akaleta maji ndani yake; akafanya kuchimba mwamba kwa chuma, akajenga visima vya kuwekea maji.[#2 Fal 20:20]
18Siku zake akaja Senakeribu, akampeleka yule amiri wake; naye akauinua mkono wake juu ya Sayuni, akamkufuru Mungu katika kiburi chake.[#2 Fal 18:13-17]
19Basi, watu wakatikisika mioyo, wakaona maumivu kama wanawake waonavyo uchungu;
20wakamwita Mungu Aliye Juu, wakimnyoshea mikono yao; naye akawasikia hima kutoka mbinguni, akawaokoa kwa mkono wa Isaya.[#2 Fal 19:15-20,35]
21Aliipiga kambi ya Waashuri,
Na malaika wake akawaangamiza.
22Maana Hezekia alifanya mapenzi ya BWANA,
Akawa hodari katika njia za Daudi.
Ambazo Nabii Isaya aliziamuru,
Aliyekuwa mkuu na amini katika njozi;
23Katika siku zake jua likarudi nyuma,[#2 Fal 20:10-11]
Hata akayaongeza maisha ya mfalme.
24Huyo aliona kwa roho ya nguvu mambo ya mwisho; akawafariji wale walioomboleza katika Sayuni.
25Akaonesha mambo yatakayokuwako hata mwisho wa nyakati, na mambo yaliyofichwa kabla hayajatokea.