Yoshua Mwana wa Sira 5

Yoshua Mwana wa Sira 5

Mafundisho kwa Maisha ya Kila Siku

1Usizitumainie mali zako,

Wala usiseme, Zanitosha basi.

2Usifuate roho yako na nguvu zako,

Kuandamana na tamaa za moyo wako.

3Usiseme, Nani atakayenitawala?

Hakika BWANA atakulipiza kisasi.

4Usiseme, Nilikosa ikanipata nini?[#Mhu 8:11]

Hakika BWANA ndiye mvumilivu.

5Kuhusu upatanisho, usiwe mjasiri wa kutenda dhambi juu ya dhambi;

6wala usiseme, Huruma zake ni nyingi, ataniachilia dhambi zangu zijapokuwa ni nyingi. Kwa sababu rehema na ghadhabu zatoka kwake, na hasira yake itawakalia wakosaji.

7Usichelewe kumrudia BWANA, wala usikawie siku kwa siku; kwa maana ghadhabu ya BWANA itatokea kwa ghafla, nawe utaangamia wakati wa kisasi.

8Wala usizitegemee mali za udhalimu, kwa kuwa hazitakufaida lolote siku ile ya hasira.

Uthabiti na kujiweza

9Usipepete kwa kila upepo,

Wala usiipitie kila njia.

10Uwe mtu thabiti wa akili,

Na liwe moja neno lako.

11Uwe mwepesi wa kusikia,

Na mzito wa kutoa jibu.

12Ikiwa unayo akili, umjibu jirani yako;

La! Huna, tia mkono wako kinywani pako.

13Heshima na aibu zina usemi,

Na ulimi humwangamiza mtu.

14Usiitwe msingiziaji,

Wala usisengenye kwa ulimi.

Juu ya mwizi inakaa aibu,

Na hukumu humsibu mnafiki.

15Usiwe fisadi katika jambo kubwa wala dogo;

Wala usipate kuwa adui badala ya rafiki.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya