Yoshua Mwana wa Sira 50

Yoshua Mwana wa Sira 50

Simoni Mwana wa Oniasi

1Mkuu wa nduguze, fahari ya watu wake,

Alikuwa Simoni mwana wa Yohana, Kuhani Mkuu.

2Wakati wake nyumba ilitengenezwa,

Na siku zake hekalu likaimarishwa;

Ukuta ukajengwa na buruji za ulinzi,

Kama zilivyo katika jumba la mfalme.

3Siku zake kiziwa kikachimbwa,

Birika lenye maji tele kama bahari.

4Akawasumbukia watu awaokoe na kutekwa,

Akajenga boma mjini mwake juu ya adui.

5Jinsi alivyotukuka akionekana hekaluni,

Alipotokea kutoka chumba cha pazia!

6Kama nyota yenye nuru kati ya mawingu,

Kama mbalamwezi katika sikukuu,

7Kama jua ling'arizapo hekalu la Mungu,

Kama upinde wa mvua katika wingu.

8Kama mawaridi wakati wa matunda mapya.

Kama nyinyoro penye mito ya maji,

Kama machipuko ya Lebanoni wakati wa joto,

9Na kama moto wa uvumba chetezoni.

Kama chombo cha dhahabu kilichofuliwa,

Kimepambwa kila namna ya vito.

10Kama mzeituni ukichanua matunda yake,

Na mzeituni mwitu wenye matawi mabichi.

11Pale pale alipovaa mavazi ya utukufu,

Na kujivika ukamilifu wa uzuri;

Alipopanda kwenye madhabahu ya enzi,

Alitukuza behewa la hekalu;

12Mwenyewe amesimama madhabahuni.

Kumzunguka, kama shada la nduguze,

Kama mierezi michanga ya Lebanoni.

Kama miti ya mitende, wamzunguka.

13Wana wa Haruni wote katika fahari yao.

Akipokea sehemu mkononi mwa nduguze,

Wanashika mikononi kafara ya BWANA,

Mbele ya kusanyiko lote la Israeli;

14Hata atakapomaliza huduma ya madhabahu,

Na kupangisha kuni mbele zake Aliye Juu;

15Na kumimina miguuni pa madhabahu

Harufu nzuri mbele zake Aliye Juu.

16Ndipo Wana wa Haruni walipopaza sauti,

Na kupiga tarumbeta zilizofuliwa;

Wakasikiza makelele ya nguvu,

Kumbukumbu mbele zake Aliye Juu.

17Ndipo watu wote walipofanya haraka,

Na kuanguka kifudifudi mpaka nchi;

Ili kusujudu mbele zake Aliye Juu,

Mbele zake Mtakatifu wa Israeli.

18Waimbaji nao wakatoa sauti zao,

Na kuhimidi kwa nguvu juu ya mkutano.

19Ndipo watu walipomsihi BWANA Aliye Juu,

Kuomba dua mbele zake Mwenye rehema;

Hata ibada ya BWANA itakapokwisha;

Na hivyo wakamaliza kuabudu.

20Ndipo aliposhuka akiinua mikono yake,[#Hes 6:24-27]

Juu ya kusanyiko lote ya wana wa Israeli;

Baraka ya BWANA i midomoni mwake,

Akajitukuza kwa kutamka YEHOVA.

21Nao wakasujudu tena mara ya pili,

Kuipokea baraka yake Aliye Juu.

Baraka

22Na sasa mhimidini Mungu wa Israeli,

Afanyaye maajabu katika dunia;

Humlea mwanadamu tangu tumboni,

Humtendea sawasawa na mapenzi yake;

23Atujalie hekima mioyoni mwetu,

Na amani iwe juu yetu daima;

24Rehema zake zithibitishwe kwetu.

Mawaidha ya Mwisho

25-26Na wakati wake atuokoe sisi.

Maneno ya mwisho

27Nimeandika kitabuni humu mafundisho ya ufahamu na elimu, mimi, Yoshua mwana wa Sira mwana wa Eleazari wa Yerusalemu, niliyeeneza hekima kwa moyo.

28Yu heri mwenye kuyatafakari haya,

Naye ayawekaye moyoni atahekimishwa;

29Akiyatenda atathibitika katika yote;

Maana kumcha BWANA ni uzima wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya