Yoshua Mwana wa Sira 8

Yoshua Mwana wa Sira 8

Baraka na Akili

1Usishindane na mkuu, usije ukaanguka mikononi mwake;

2usipingane na tajiri, asije akakuweza kama labda itakavyotukia; kwa maana dhahabu imewaharibu wengi, na kuipotosha mioyo ya wafalme.

3Usijadiliane na mtu mwenye maneno mengi, ukaongeza kuni juu ya moto wake;

4wala usibishane na mfidhuli, wazee wako wasipate kutukanwa.

5Usimshutumu mtu akiiacha dhambi yake; kumbuka ya kwamba sisi sote tunastahili adhabu.

6Usimdharau mtu katika uzee wake, mradi miongoni mwetu wengine tunazeeka;

7pia usisimange juu yake aliyefariki; kumbuka ya kwamba miongoni mwetu sisi sote tunakufa.

Mapokeo

8Usijitenge na mazungumzo ya wenye hekima, bali ujizoeze na mithali zao; yaani, kwa hizo utajifunza elimu, na jinsi ya kusimama mbele ya wakuu.

9Usikatae maongezi ya wazee, ambao walijifunza kwa baba zao; maana kwa hayo utapata ufahamu, na kutoa jawabu ikiwapo haja.

Busara

10Usichochee makaa ya mkosaji, usije ukaungua katika mwako wa moto wake.

11Usijiinue mbele ya mwenye jeuri, asije akayavizia maneno ya kinywa chako.

12Usimkopeshe yeye aliye mkuu kuliko wewe; la! Umemkopesha, ujifanye kama mtu aliyepoteza.

13Usiwe mdhamini kupita kadiri yako la! Umedhamini, ujifikiri kama aliyeshurutishwa kulipa.

14Usishitakiane na hakimu; kwa sababu minajili heshima yake atapewa haki.

15Usiende njiani pamoja na jabari, asije akauonea uchungu; huyo atafanya kama apendavyo, nawe utapotea katika ujinga wake.

16Usipigane na mtu wa ghadhabu, wala usisafiri naye jangwani; kwa kuwa damu si kitu kwake, na pasipopatikana msaidizi atakuangamiza.

17Usishauriane na mpumbavu, ambaye hataweza kuficha siri yako;

18usifanye jambo la siri mbele ya mgeni, mradi hujui atakalofanyiza;

19wala usiufunue moyo wako kwa kila mtu; wala usimwache mtu akulipe fadhili.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya