Yoshua Mwana wa Sira 9

Yoshua Mwana wa Sira 9

Mashauri kuhusu Wanawake

1Usimwonee wivu mkeo akaaye kifuani pako, ukamfundisha fundisho baya juu yako mwenyewe.[#Hes 5:12-15]

2Usimpe mwanamke yeyote uhai wako, hata azikanyage nguvu zako.

3Usimlaki mwanamke mgeni, usije ukanaswa naye kwa nasibu.

4Usiandamane na mwanamke aliye malenga, ama yamkini utategwa kwa hila zake.

5Usimkodolee macho msichana, ama utatatanishwa katika madai yake.

6Usiwape malaya uhai wako, usije ukapotewa na urithi wako.

7Usitazame huku na huku katika njia za mji, wala usitembee ndani yake panapo ukiwa.

8Jicho lako uligeuzie mbali na mwanamke mrembo, wala usiukazie macho uzuri wa mwingine; wengi wamepotoshwa kwa uzuri wa wanawake, na kwa huo ashiki huwashwa kama moto.

9Usiketi sebuleni pamoja na yeye aliyeolewa, wala usiende mandari naye kwenye mvinyo; moyo wako usije ukamgeukia, na roho ikateremkia upotevu.

Uchaguzi wa Marafiki

10Rafiki wa zamani usimwache, madhali rafiki mpya hatalingana naye; rafiki mpya afanana na divai mpya, iwapo imekomaa utainywa kwa furaha.

11Usihusudu fahari yake mwenye dhambi, mradi hujui ni nini itakayomwangusha.

12Usiyafurahie mema yao wasio haki; kumbuka ya kwamba hawatashuka kaburini bila adhabu.

13Ukae mbali naye mwenye amri ya kuua, hivyo hutaionja hofu ya kuuawa; aidha, ukiwa umemjia, usifanye kosa asije akakufisha; uwe macho kwamba unakwenda katikati ya matanzi, na mfano wa kukanyaga buruji za ngome.

14Kadiri uwezavyo uwakisie jirani zako, na kushauriana na wataalamu;

15maongezi yako na yawe kwao walio na akili, na mazungumzo yako katika sheria yake Aliye Juu.

16Wenye haki na wawe waizungukao meza yao; na kujisifu kwako kuwe katika kumcha BWANA.

Kuhusu Watawala

17Kazi ya mikono itasifiwa kwa ustadi wa mafundi; na mwenye kutawala watu atahesabiwa hekima kwa usemi wake.

18Mwenye maneno mengi ni hatari katika mji, naye anenaye bila kufikiri ndiye atakayechukiwa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya