Tito 2

Tito 2

Toa mafundisho mema

1Lakini wewe, nena mambo yanayoambatana na mafundisho mema;[#1 Tim 6:3; 2 Tim 1:13]

2ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika subira.[#1 Tim 5:1]

3Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wanaofundisha yaliyo mema;[#1 Tim 3:11]

4ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;

5na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.[#Efe 5:22]

6Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi;

7katika mambo yote ukijionesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionesha usahihi na ustahivu,[#1 Tim 4:12; 1 Pet 5:3]

8na maneno yafaayo yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.[#1 Pet 2:15]

9Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wakaidi,[#Efe 6:5; 1 Tim 6:1; 1 Pet 2:18]

10wasiwe wezi; bali wauoneshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mungu aliye Mwokozi wetu katika mambo yote.[#Tit 1:3]

11Maana neema ya Mungu iwaokoao wanadamu wote imefunuliwa;

12nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;[#Efe 1:4; 1 Yoh 2:16]

13tukilitazamia tumaini lenye baraka na kufunuliwa kwa utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;[#1 Kor 1:7; Rum 5:2; Flp 3:20]

14ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wake mwenyewe walio na bidii katika matendo mema.[#Kut 19:5; Kum 4:20; 7:6; 14:2; Zab 130:8; 1 Pet 2:9; 3:13; Gal 1:4; 1 Tim 2:6; Efe 2:10; Eze 37:23]

15Nena mambo hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.[#1 Tim 4:12]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya