Tobiti 10

Tobiti 10

Mahangaiko ya wazazi wa Tobia

1Huko nyuma kila siku baba yake Tobiti alikuwa akizihesabu siku; na siku za safari zilipotimia, wala hawajaja.

2Alisema, Je! Labda wamekawilishwa? Ama labda Gabaeli amekufa, wala hakuna mtu wa kumpa fedha?

3Akahuzunika mno.

4Lakini mkewe akamwambia, Mwanangu amekufa; tazama, alivyokawia. Akaanza kumwombolezea, akasema.

5Ole wangu! Mwanangu; tangu siku nilipokuachia usafiri; wewe uliye nuru ya macho yangu!

6Tobiti akamwambia, Nyamaza, usifadhaike; yu mzima.

Tobia na Sara Waondoka Ekbatana

7Akamwambia, Nyamaza wewe, usinidanganye, mwanangu amekufa. Naye hutoka kila siku kwenda katika njia waliyoiendea; wala hakula chakula mchana kutwa: wala hakukoma usiku kucha kumwombolezea mwanawe Tobia; hata zilipotimia zile siku kumi na nne za karamu ya arusi, ambazo Ragueli amemwapia akae huko siku hizo. Ndipo Tobia alipomwambia Ragueli, Niruhusu niende, maana baba yangu na mama yangu wanakata tamaa ya kuniona tena.

8Lakini mkwewe akamwambia, Afadhali ukae, nami nitatuma watu kwa baba yako; nao watampasha habari zako.

9Bali Tobia akamjibu, Sivyo kabisa; bali uniruhusu niende kwa baba yangu.

10Kwa hiyo Ragueli akaondoka akampa mkewe Sara, na nusu ya mali zake, watumishi na ng'ombe na fedha.

11Akawabariki, akawaruhusu, akasema, Wanangu, Mungu wa mbinguni akujalieni uheri kabla sijafa.

12Akamwambia binti yake, Waheshimu wakwezo, walio sasa kama wazazi wako; ili nipate sifa zako njema. Akambusu. Edna naye akamwambia Tobia, Ndugu yangu mpenzi, Mungu wa mbinguni akurudishe, na anijalie kuwaona watoto wako atakaokuzalia binti yangu Sara, ili nifurahi mbele za BWANA. Angalia, nimekukabidhi binti yangu amana bora, maana usimchokoze.

13Baada ya hayo Tobia akaenda zake, hali akimhimidi Mungu kwa kuwa ameifanikisha safari yake. Akawabariki Ragueli na mkewe Edna.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya