The chat will start when you send the first message.
1Halafu yake Tobiti akamwita mwanawe Tobia, akamwambia, Mwanangu, angalia mtu huyu aliyefuatana nawe alipwe mshahara wake, na lazima uongeze.
2Akamwambia, Baba, si hasara kwangu kumpa nusu ya zile mali nilizozileta.
3Kwa maana amenirudisha kwako salama; akamponya mke wangu; akaniletea ile fedha; akakuponya na wewe pia.
4Mzee akasema, Ni haki.
5Basi akamwita malaika, akamwambia, Afadhali sana wewe utwae nusu ya yote mliyoleta.
6Ndipo alipochukua wote wawili kwa faragha, akawaambia, Mhimidini Mungu, na kumshukuru, na kumwadhimisha; na kumpa shukrani mbele ya wote walio hai kwa mambo yote aliyowatendeeni. Ni vema kumhimidi Mungu na kulikuza jina lake; na kuyatangaza kwa heshima matendo ya Mungu. Basi msilegee katika kumshukuru.
7Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu. Mtende yaliyo mema, na mabaya hayatawapata.
8Bora ni kusali pamoja na kufunga na kutoa sadaka za haki. Kidogo pamoja na haki ni bora kuliko wingi pasipo na haki. Yafaa kutoa sadaka kuliko kuweka akiba ya dhahabu.[#Sira 29:8-13]
9Sadaka huokoa na mauti, nazo zitasafishia mbali dhambi zote. Watoao sadaka na kutenda haki watajaa uzima,[#Mit 11:4; Dan 4:27; Sira 3:30]
10bali watendao dhambi ni adui za uhai wao wenyewe.
11Hakika sitawaficheni neno. Nimesema, Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu.
12Basi hapo mliposali, wewe na mkweo Sara mimi niliupeleka ukumbusho wa sala zenu mbele zake Aliye Mtakatifu; na hapo ulipowazika wafu, nilikuwapo pamoja nawe vile vile.[#Ayu 33:23-24; Mdo 10:4; Ufu 8:3-4]
13Na hapo usipokawia kuondoka na kuacha chakula chako, ili uende kumzika yule mfu, tendo lako jema halikufichwa kwangu; lakini nilikuwapo pamoja nawe.
14Na sasa Mungu amenituma ili niwaponye, wewe na mkweo Sara.
15Mimi ndimi Rafaeli, mmojawapo wa malaika watakatifu saba, wapelekao sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake Aliye Mtakatifu.[#Zek 4:10; Lk 1:19; Ufu 8:2]
16Mara wakafadhaika wote wawili, wakaanguka kifudifudi; kwa maana waliogopa.
17Akawaambia, Msiogope, amani kwenu, mhimidini Mungu milele.
18Maana sikuja kwa hisani yangu, bali nilikuja kwa mapenzi ya Mungu wetu. Kwa hiyo mhimidini Yeye milele.
19Siku hizi zote nilionekana nanyi, lakini sikula wala sikunywa, ila ninyi mliona njozi.
20Sasa mshukuruni Mungu; kwa kuwa mimi ninapaa kwake aliyenituma; nanyi andikeni katika kitabu mambo yote yaliyotendeka. Nao walipoondoka hawakumwona tena.
21Wakayakiri matendo makuu ya ajabu ya Mungu, na jinsi Malaika wa BWANA alivyowatokea.