The chat will start when you send the first message.
1Siku ile Tobiti aliikumbuka ile fedha aliyoiweka amana kwa Gabaeli huko Rage, mji wa Umedi.
2Akasema nafsini mwake, Nimetaka kufa; mbona nisimwite mwanangu Tobia, ili nimwarifu habari za ile fedha kabla sijafa.
3Alipomwita akamwambia, Mwanangu, nitakapokufa unizike; tena usimdharau mama yako; bali umheshimu siku zote za maisha yako, ukayatende yampendezayo, wala usimhuzunishe.
4Mwanangu, ukumbuke ya kuwa alipatwa na hatari nyingi kwa ajili yako, ulipokuwamo tumboni mwake. Naye akiisha kufa, umzike pamoja nami katika kaburi moja.
5Mwanangu, umkumbuke BWANA, Mungu wetu, siku zako zote; wala usikaze nia yako kutenda dhambi, wala kuzivunja amri zake; utende kwa unyofu maisha yako yote, wala usizifuate njia za uovu.
6Kwa maana ukitenda kwa kweli matendo yako utakufanikiwa, nao wote watendao kwa haki watafanikiwa.
7Toa sadaka katika mali zako; wala utoapo sadaka jicho lako lisiwe na choyo; wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini, nawe hutageuziwa mbali uso wa Mungu.[#Kum 15:7-8; Mit 19:17; Sira 3:30—4:6; 1 Yoh 3:17]
8Ukiwa na wingi utoe sawasawa na wingi wako; ukiwa na kidogo tu usiogope kutoa sawasawa na kidogo hicho.
9Kwa maana wajiwekea hazina bora kwa siku ya dhiki.
10Madhali sadaka huokoa na mauti, wala hazimwachi mtu afike gizani.
11Sadaka ndizo thawabu bora kwao wote wazitoazo usoni pake Aliye Juu.
12Mwanangu, ujihadhari na ukahaba; na zaidi ya hayo ujitwalie mke katika uzao wa baba zako; wala usijitwalie mwanamke mgeni asiye wa kabila ya baba yako. Maana sisi tu wana wa manabii. Mwanangu, ukumbuke; Nuhu, Abrahamu, Isaka, Yakobo, baba zetu tangu mwanzo; wote walioa watu wa jamaa zao wenyewe; wakabarikiwa katika watoto wao; na uzao wao utairithi nchi.
13Basi sasa, mwanangu, uwapende ndugu zako, kwa kumchukua mke aliye wa kwao; wala moyoni mwako usiwadharau ndugu zako, wana na binti za watu wako. Maana katika dharau kuna uharibifu na udhia mwingi, na katika upotovu kuna upunguo na uhitaji mwingi; mradi upotovu huzaa njaa.
14Mshahara wa mtu yeyote aliyekufanyia kazi usikae nao, bali umpe mara; maana wewe ukimtumikia Mungu, Yeye atakulipa. Mwanagu, uwe na hadhari katika matendo yako yote, pia uwe na busara katika mwenendo wako.
15Na yale uyachukiayo mwenyewe usimtende mtu yeyote kama yale. Usijilevye kwa mvinyo, wala mlevi asifuatane nawe katika njia yako.
16Wenye njaa uwape baadhi ya chakula chako, na walio uchi uwape baadhi ya nguo zako; sawasawa na wingi wako utoe sadaka; wala utoapo sadaka jicho lako lisiwe na choyo.
17Utoe chakula kwa ukarimu kwenye maziko ya wenye haki; lakini waovu usiwape kitu.[#Kum 26:14]
18Utake shauri kwa kila mtu aliye na hekima, wala usilidharau shauri la kufaa lenye njia.
19Umhimidi BWANA, Mungu wako, siku zote. Umwombe Yeye ili njia zako zinyoshwe, na mapito yako yote na mashauri yako yote yafanikiwe; maana katika mataifa hakuna lenye shauri; bali BWANA mwenyewe ndiye atoaye mema yote, naye humdhili yeyote atakaye na kama atakavyo. Basi, mwanangu, uyakumbuke mausia yangu, wala usiyaache kufutika katika nia yako.
20Na sasa nakuarifu habari ya kuwa nilimkabidhi Gabaeli mwana wa Gabria talanta kumi huko Rage, mji wa Umedi.
21Wala usihofu, mwanangu, ya kuwa tumekuwa maskini; maana una mali nyingi, huku ukimcha Mungu, na kujiepusha na dhambi zote, na kutenda mambo yale yampendezayo machoni pake.[#1 Tim 6:6-8]