The chat will start when you send the first message.
1Walipokwisha kula wakamwingiza Tobia kwake.
2Naye alipokuwa akienda, akayakumbuka maneno ya Rafaeli, akayatwaa majivu ya ubani, akavitia juu yake moyo na ini vya samaki, akafukiza moshi.
3Yule jini alipoisikia harufu, akakimbia hata kukimbilia pande za juu za Misri; huko ndiko malaika alikomfunga.[#Mt 12:43]
4Na wakiisha kuwamo chumbani wote wawili. Tobia akaondoka kitandani, akasema, Ndugu yangu, ondoka, ili pamoja tumwombe Mungu atuhurumie.
5Ndipo Tobia alipoanza kusema, Ee Mungu wa baba zetu, umehimidiwa; na jina lako takatifu tukufu limehimidiwa milele; mbingu nazo zikuhimidi, pamoja na viumbe vyako vyote.[#Dan 10:12]
6Ndiwe uliyemuumba Adamu, ukampa mkewe Hawa, ili awe msaidizi na tegemeo; na kwao umetoka uzao wote wa wanadamu. Nawe ukasema, Si vema mwanamume akae peke yake; na tumfanyizie msaidizi wa kufanana naye.[#Mwa 24:55]
7Na sasa, Ee BWANA, simtwai huyu ndugu yangu kwa ajili ya tamaa, bali katika kweli. Uamuru nirehemiwe, hata niwahi kuona uzee pamoja naye.
8Sara akasema pamoja naye, Amin.
9Basi usiku ule wakalala usingizi wote wawili. Ragueli akaondoka mapema, akaenda akachimba kaburi;
10akasema, Huenda huyu naye atakufa.
11Ragueli akarudi nyumbani, akamwambia mkewe Edna,
12Tuma mjakazi mmoja, amtazame kama yu hai. La! Amekufa, na tumzike; wala asijue mtu yeyote.
13Basi yule mjakazi akaufungua mlango, akaingia; akawakuta wote wawili wamelala.
14Akatoka akawaambia ya kwamba yu hai.
15Mara Ragueli akamhimidi Mungu, akasema, Ee Mungu, umehimidiwa kwa sifa zote zilizo safi takatifu; kwa hiyo watakatifu wakuhimidi, pamoja na viumbe vyako vyote, na malaika wako wote; na wateule wako wote wakuhimidi milele.
16Wewe umehimidiwa kwa kuwa umenifurahisha; wala yale niliyoyahofu hayakunipata; bali umetutendea sawasawa na rehema zako nyingi.
17Wewe umehimidiwa kwa kuwa umewarehemu wawili hawa, walio watoto pekee wa wazazi wao. Ee BWANA, uwajalie rehema, ili waimalize maisha yao katika afya, pamoja na furaha na rehema.
18Kisha Ragueli akawaamuru watumishi wake walifukie kaburi.
19Akaifanya karamu ya arusi yao siku kumi na nne.
20Na kabla ya kuisha siku za karamu ya arusi, Ragueli akamwapisha Tobia asiondoke hata siku zile kumi na nne za karamu ya arusi zitimie.[#Mwa 24:55]
21Baadaye aitwae nusu ya mali zake zote, aende salama kwa baba yake; akasema, Na iliyobaki utapewa nitakapokufa mimi na mke wangu.