The chat will start when you send the first message.
1Pendeni haki, enyi waamuzi wa dunia;[#Hek 6:1-11]
Tafakarini habari za BWANA kwa moyo mwema,
Na kumtafuta katika unyofu wa moyo.
2Kwa sababu huonekana nao wasiomjaribu, na kufunuliwa kwao wasiokosa kumwamini.
3Mradi fikira zilizopotoka hutenga wanadamu na Mungu, na enzi yake ikijaribiwa, huwafadhaisha wajinga.
4Hekima haiingii katika roho ya mtu awazaye maovu, wala haikai katika mwili wa mtu aliyefungwa rehani na dhambi.
5Kwa kuwa roho takatifu yenye maadili huikimbia hila, hubumburuka kujiepusha na fikira zisizo na akili, hufadhaika kuingiwa na udhalimu.
6Maana hekima ni roho ambayo huwapenda wanadamu, wala haimwachilii mkufuru hatia ya midomo yake; kwa sababu Mungu huvishuhudia viuno vyake, na kuusimamia hasa moyo wake, na kuusikiliza ulimi wake.
7Roho ya BWANA imeujaza ulimwengu, nayo inayoviungamanisha viumbe vyote hujua maana ya kila sauti.
8Kwa hiyo kila anenaye yasiyo haki hafichiki kabisa, wala Haki haimpiti ikifanya hukumu.
9Yaani, katikati ya mashauri yake mtu mwovu atachunguzwa, na sauti ya maneno yake itamfikia BWANA, ili maasi yake yahukumiwe.
10Ndiyo maana kuna sikio la wivu ambalo husikiliza yote, wala kelele za manung'uniko hazisitiriki.
11Jihadharini, basi, na manung'uniko yasiyofaa, na kujizuia ndimi zenu na masingizio; madhali neno linenwalo kwa siri haliendelei bure, na kinywa kisemacho uongo huiangamiza roho.
12Msijitakie mauti katika ukosefu wa roho zenu;
Wala msijivutie uharibifu kwa kazi za mikono yenu.
13Yaani, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea.[#Eze 18:32; 33:11; 2 Pet 3:9]
14Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yoyote ya uharibifu, wala ahera.
15Maana haki yaishi milele.
16Lakini wanadamu wasio haki, kwa mikono yao na kwa maneno yao, walijiitia mauti; wakaifanya rafiki, wakadhoofu; wakaagana nayo kwa sababu wamestahili kutiwa katika fungu lake.[#Mit 8:36; Isa 28:15; Sira 14:12]