The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kidogo hatia yao, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema;
2wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, BWANA.
3Yakini kwa habari za Wakanaani, wenyeji wa kale wa nchi takatifu,[#Kum 12:31; 18:9-13]
4ulichukizwa nao kwa sababu walijishughulisha na kazi makuruhi za usihiri na kawaida za unajisi,
5wakichinja watoto bila huruma, na kula watu, nyama na damu pia, kuwa sadaka;
6washiriki wa chama cha kukufuru, na wauaji wa wachanga wao wenyewe wasiokuwa na msaada; ukafanya shauri la kuwaangamiza kwa mikono ya baba zetu;
7ili nchi ile, iliyo ya thamani hasa machoni pako kuliko nchi zote, ipokee jamii ya watu waliostahili kuwa watumishi wa Mungu.
8Hata hivyo uliwaachilia kwa kuwa ni wanadamu, ukatangulia kupeleka manyigu, wawe watakadamu wa majeshi yako, ili kuwaangamiza kidogo kidogo.[#Kut 23:28]
9Si kana kwamba hukuweza kuwatiisha wale waovu vitani kwa mkono wa wenye haki, au kwa wanyama wakali mno, na kuwafutia mbali mara kwa neno moja tu lenye nguvu;
10lakini uliwapa nafasi ya kutubu, hapo ulipokuwa ukiwahukumu kidogo kidogo; tena ulijua ya kwamba wale wamezaliwa waovu kwa asili, maumbile yao ukorofi, na mawazo yao yasiyoweza kubadilika kamwe.
11Mradi walikuwa uzao uliolaaniwa tangu awali. Aidha, hukuwaachilia dhambi zao kwa hofu ya yeyote.
12Kwa maana ni nani atakayekuambia Wewe, Umefanyaje? Kisha ni nani atakayeipinga hukumu yako? Naye ni nani atakayekushitaki kwa kuwa mataifa uliowafanya Wewe wamepotea? Au ni nani atakayekuja na kusimama mbele zako ili kukulipiza kisasi kwa ajili ya waovu?
13Maana hakuna Mungu mwingine yeyote ila Wewe, unayewaangalia watu wote, hata umwoneshe huyo ya kuwa hukuhukumu bila haki;
14wala hakuna mfalme yeyote, wala mkuu yeyote, atakayeweza kuonana nawe uso kwa uso, ili awatetee wale uliowaadhibu.
15Lakini Wewe u Haki, nawe unavitawala vitu vyote kwa haki, ukiona ya kwamba haikuhusu uweza wako kumtia hatiani mtu moja asiyestahili mwenyewe kuadhibiwa.
16Madhali ndio uweza wako ulio asili ya haki, na kwa sabiki ya milki yako juu ya mambo yote unawaachilia wote.
17Kwa kuwa iwapo wanadamu hawasadiki ya kuwa umekamilika katika uweza wako, Wewe wazidhirisha nguvu zako; tena ukijishughulisha na wale wasioikiri kweli hiyo, waifadhaisha jeuri yao.
18Lakini desturi yako unauzuia hata uweza wako, na kuhukumu kwa upole, na kututawala kwa uvumilivu mwingi. Yaani uweza unao, wakati wowote utakapo kuutumia.
19Pamoja na hayo, uliwafundisha watu wako kwa matendo yako ya namna hiyo ya kwamba imempasa mwenye haki kuwa mpenda wanadamu; tena ukawatilia wanao tumaini jema, kwa sababu endapo watu wametenda dhambi, unawajalia toba.
20Yaani, ikiwa, kwa habari ya wale adui za watumishi wako waliostahili kufa, uliwalipiza kisasi kwa uangalifu huo mwingi na rehema (maadamu uliwajalia muda na nafasi ya kujiepusha na uovu wao):
21kwa uangalifu kama nini uliwahukumu wanao, ambao uliwapa baba zao nyapo na maagano ya ahadi njema!
22Kwa hiyo, pindi unapoturudi sisi, unawapiga adui zetu mara kumi elfu zaidi; ili makusudi sisi tupate kuutafakari wema wake tunapohukumu, na kutazamia rehema tunapohukumiwa.
23Na kwa ajili ya hayo yote uliwatesa wale Wamisri walioishi maisha ya upumbavu kwa njia ya machukizo yao wenyewe.
24Maana yakini walitangatanga sana katika njia za ukosefu, wakidhania kuwa miungu hata vinyama vile vilivyodharauliwa kati ya adui zao, wakadanganyika mfano wa watoto wachanga wasio na akili.
25Hivyo, kana kwamba ni watoto wasio na akili, uliwaletea hukumu zako ili kuwadhihaki.
26Lakini wale wasiotaka kupokea maonyo, huku wakirudiwa kwa dhihaka kama watoto, watapatwa na hukumu ya namna inayomhusu Mungu.
27Kwa maana wale walioadhibiwa kwa njia ya viumbe vile walivyovidhania kuwa ni miungu, na kwa misiba ile waliyoionea uchungu walimfahamu Yeye ambaye kwanza wamekataa kumjua, ila wakamtambua kuwa ndiye Mungu wa kweli. Na kwa hiyo ukomo wa kuhukumiwa uliwaangamiza piapia.