Hekima ya Sulemani 14

Hekima ya Sulemani 14

Upumbavu wa nahodha kuomba miungu

1Tena, kuna mtu anayejiweka tayari kusafiri jahazini, endapo anataka kufanya safari yake juu ya maji yaumkayo, naye hulitia gogo la mti, bovu kabisa kuliko jahazi itakayomchukua!

2Kwa maana jahazi ile ilibuniwa kwa tamaa ya faida; na fundi akaiunda kwa akili zake;

3ila maongozi yako, Baba, ndiyo yanayoiongoza njiani. Kwa sababu hata baharini umetupa njia, na katikati ya mawimbi kuna mapito ya salama.

4Ukituonesha ya kwamba unaweza kuokoa katika kila hatari, hata na mtu asiye na ufundi huo aweza kung'oa nanga.

5Nayo ni mapenzi yako kazi za hekima yako zisikae bure; kwa hiyo watu huyaaminisha maisha yao kwa kipande kidogo cha mti, na kwa kupitia msukosuko wa bahari hata juu ya chelezo cha mbao huletwa salama mpaka pwani.

6Hata na siku za kale pia, wale majitu wenye kiburi walipokuwa wakiangamia, Nuhu, yule mtu aliyekuwa tumaini la ulimwengu alikimbilia safina, na, kwa kuwa mkono wako ulishika usukani, akawaachia wanadamu mbegu ya vizazi vitakavyokuja.

7Kwa maana kimebarikiwa kile kipande cha mti, ambacho kwa njia yake kumekuja wokovu.

8Lakini sanamu iliyofanyika kwa mikono imelaaniwa, naam, sanamu na yeye aliyeifanya pia; kwa sababu kuifanya kulikuwa kazi yake, na kile kitu kinachoharibika kimeitwa mungu.

9Maana mfanyaji aliye mwovu na uovu wake pia ni makuruhu machoni pa Mungu;

10naam, hakika yake kitendo kitaadhibiwa pamoja na yule aliyekitenda.

11Kwa hiyo katikati ya sanamu za mataifa kutakuwa na mapatilizo; kwa sababu, ingawa zimefanyizwa katika viumbe alivyoviumba Mungu, zimefanyizwa kuwa machukizo, na vikwazo mbele ya roho za watu, na matanzi kwa miguu ya wapumbavu.

Mwanzo na maovu ya kuabudu sanamu

12Kwa maana kubuni sanamu kumekuwa chanzo cha uasherati, na uvumbuzi wake ni uharibifu wa maisha.

13Mradi hizo hazikuwako tangu awali, wala hazitakuwako hata milele;

14yaani ziliingia ulimwenguni kwa majivuno ya wanadamu, na kwa hiyo zimeamriwa mwisho wake utakaokuja kasi.

15Kwa kuwa baba mmojawapo aliyetaabika kwa majonzi yasiyotazamiwa, akifanya sanamu ya mtoto wake ambaye amefariki mapema, angeweza halafu kumstahi kama mungu yeye aliyekuwa kwanza binadamu aliyekufa tu, na kuwakabidhi wale waliokuwa chini yake madhehebu mengineyo na kanuni za ibada.

16Baadaye desturi hiyo ya upotevu, ikithibitishwa baada ya miaka kupita, hushikwa kuwa sheria;

17hata kwa amri ya wakuu sanamu za kuchonga zikaabudiwa. Tena, hapo wasipoweza kumheshimu mfalme hadharani, kwa sababu walikuwa wakikaa mbali sana, wakiwazia sura yake hapo walipo mbali, watu walifanyiza sanamu iliyoonekana ya mfalme huyo waliyemheshimu; ili kwa juhudi yao wapate kujipendekeza kwake yeye asiyekuwapo, kana kwamba amekuwapo.

18Hata na zaidi ya hayo, watu wasiomjua waliongeza ibada yao, wakiwa wameshawishiwa kwa jitihada ya mchonga sanamu;

19maana yeye, akitaka labda kumpendeza mwenye mamlaka, alitumia ufundi wake katika kuuzidisha uzuri wa sura hiyo;

20na makutano, wakivutwa kwa uzuri wa kazi yake, halafu walimdhania kuwa ni mungu wa kuabudiwa, yeye aliyekuwa kwanza akiheshimiwa kama mtu tu.

21Basi, jambo hilo likawa kikwazo cha maisha, kwa jinsi watu, wakishurutishwa ama kwa maafa, ama kwa usultani, walivyotaja mawe na miti kwa jina lile lisiloshirikika.

Mapato ya ibada za sanamu

22Baadaye haikutosha watu wasipotoshe njia zao katika habari za kumjua Mungu; lakini zaidi ya hilo, wakiishi katika hali ya taabu kubwa kwa sababu ya kutokumjua, wamekosea juu ya umati wa maafa ambao huutajia amani.

23Kwa maana, ama kwa kuua watoto katika ibada zao, ama kwa kuzishika ibada zilizo za siri kabisa, ama wakienda mandari zenye wazimu zilizo za kigeni,

24wameacha hata kuuheshimu uhai, au usafi wa ndoa; bali mtu mmoja aweza kumletea mwenzake ama kufa kwa hila, ama uchungu wa kupata mwana wa haramu.

25Tena, mambo yote yameingia fujo, yamejaa damu na uuaji, kuiba na kudanganya, ufisadi, uongo, ghasia, zuri, zahama,

26utovu wa shukrani kwa fadhili zilizopokewa, kuzinajisi roho za watu, kuburuga hali ya kiume na kike, machafuko ya ndoa, uzinzi na uasherati.

27Madhali kuziabudu zile sanamu zisizo halali hata kuzitaja ni chanzo, na sababu, na kusudi, la kila lililo ovu.

28Maana wale waziabuduo hujifurahisha kwa wazimu, au kutabiri uongo, au huishi wenyewe katika ufasiki; tena huapa kwa uongo bila kufikiri,

29kwa kuwa wanazitumainia sanamu zisizo na uhai, na wakiisha kuapa kwa upotoe wanatazamia ya kuwa hawapata hasara yoyote.

30Lakini kwa malipo ya dhambi hizo mbili watu wale watafuatiwa na Haki, maana kwa kustahi sanamu walimwazia Mungu mawazo mabaya, pia wakaapa katika udhalimu na hila kwa sababu wanaudharau utakatifu.

31Lakini si nguvu ya viumbe vile ambavyo watu huapa kwa kuvitaja, ila ndiyo Haki inayowachungulia wakosaji; nayo sikuzote huupatiliza udhalimu wa wabaya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya