Hekima ya Sulemani 16

Hekima ya Sulemani 16

Misri na Israeli: Wanyama balaa na kware

1Kwa sababu hiyo Wamisri waliadhibiwa ilivyostahili kwa njia ya viumbe vya namna hiyo, na kuteswa kwa wingi wa watambazi.

2Ila Wewe, badala ya adhabu, uliwapa Waisraeli fadhili, na kuwawekea tayari kware kwa chakula cha namna ya kigeni ya kuonja, kwa kadiri ya tamaa ya roho zao.[#Kut 16:11-13; Hes 11:31-32]

3Ili makusudi wale adui wakitamani chakula, wakirihike na tamaa kwa kioja cha vyura, vile viumbe walivyopolekewa; bali hao watu wako, waliopungukiwa chakula kwa muda mchache, washirikishwe hicho chakula kigeni.

4Kwa kuwa iliwapasa wale kwamba wajiliwe katika udhalimu wao na uhitaji usioepukika, bali hao waoneshwe tu jinsi adui zao waliovyoteswa.

Misri na Israeli: Nzige na nyoka ya shaba

5Mradi hao walipojiliwa na ukali utishao wa hayawani, na kuwa katika kuangamizwa kwa kuumwa na nyoka, hata hivyo hasira yako haikudumu upeo;[#Hes 21:6-9]

6ila kwa kuwaonya walisumbuliwa kipindi, wenye ishara ya wokovu ili kuwakumbusha maagizo ya sheria yako;

7kwa kuwa yeye aliyegeukia nyoka ya shaba aliokoka, si kwa ajili ya hiyo iliyoonekana, bali kwa ajili yako Wewe, uliye Mwokozi wa wote.

8Naam, na kwa njia hii uliwahakikisha adui zetu ya kwamba ndiwe uokoaye katika kila baya.

9Maana wale adui, kuumwa na nzige na mainzi kuliwaua, isionekane njia ya kuponya maisha yao, maana wamestahili kuadhibiwa na vidudu hivyo,

10bali watoto wako, hata meno ya majoka yenye sumu hayakuwaweza, maana kwa rehema zako uliwapitia walipokuwapo, ukawaponya.

11Mradi waliumwa ili makusudi kuwakumbusha maagizo yako na kuponywa upesi wasije wakaanguka katika usahaulifu mzito, hata wasiweze kusaidiwa kwa fadhili zako.

12Kwa kuwa hakika waliponywa, si kwa mti wala dawa ya kubandika yenye kutuliza maumivu, bali kwa neno lako, BWANA, lenye kuponya yote.

13Madhali Wewe unayo mamlaka juu ya uhai na mauti, wateremsha mpaka malango ya kuzimu, na kuleta juu tena.

14Hivyo hata mtu awezaye kuua katika ukorofi, hawezi kuirudisha roho ilikwisha kutoka, wala kuiweka huru roho iliyokaribishwa kutoka, wala kuiweka huru roho iliyokaribishwa kuzimuni.

Dhoruba ya hatari yapiga Misri

15Lakini haiwezekani kujiepusha na uweza wako.

16Kwa maana wale wakorofi wa Misri waliokataa kukujua walipigwa kwa nguvu za mkono wako, wakafuatiwa na mvua za kigeni na mvua za mawe, na tufani zisizozuilika, wakateketezwa kabisa na moto;

17tena, nayo ni ajabu kupita yote, katika maji yawezayo kuzimisha yote moto ukazidi kuwaka kwa nguvu; madhali ulimwengu huwapigania wenye haki.

18Kwa maana wakati huu mwali ulipungukiwa na ukali wake, usivichome vile viumbe vilivyopelekwa juu ya wadhalimu, ila wale wenyewe watazame na kuona ya kwamba wamefuatiwa na hukumu ya Mungu;

19tena wakati huu uliwaka hata ndani ya maji kupita nguvu za moto, ili kuyaharibu mazao ya nchi ile isiyo haki.

Waisraeli wapokea mana

20Badala ya hayo uliwapa watu wako chakula cha mashujaa ili wale, na mkate toka mbinguni uliwawekea tayari bila kazi yao, chakula kilicho kitamu na cha kupendeza tamaa ya kila mtu.[#Kut 16:1-36]

21Kwa maana kitu chenyewe kiliudhihirisha utamu wako kwa watoto wako, na kwa kushibisha shauku ya mlaji kikajichanganya kama kila mtu alivyochagua.

22Walakini kile kilichofanana na theluji au barafu kilistahimili moto bila kuyeyuka, ili watu wapate kujua ya kwamba moto ulikuwa ukiharibu mazao ya adui, ukiwaka katika mvua ya mawe na kumulika ndani ya mvua;

23pia moto huo ukawa umesahau uwezo wake, ili wenye haki washibe.

24Madhali ulimwengu, ukikutumikia Wewe, Mola wetu, huuzidisha uwezo wake juu ya wasio haki, ili kuwarudi, tena huupunguza kwa ajili yao wakutumainio, ili kuwafadhili.

25Kwa hiyo wakati ule nao moto ukajigeuza kuwa wa kila aina, ukakutumikia Wewe unayeyahifadhi mambo yote katika wema wako, kwa kadiri ya tamaa yao waliokuwa na haja;

26ili watoto wako, BWANA, uwapendao, wajifunze ya kwamba si mazao ya matunda ya ardhi yanayomlisha mtu, ila kwa neno lako wakutumainio huhifadhika.

27Kwa maana kile kitu, kiitwacho mana, kisichoharibika kwa moto, kiliyeyuka kwa kupata moto wa kiango dhaifu cha jua;

28ili ijulike ya kama imetupasa kuamka kabla ya jua ili kukushukuru, na kukuomba dua wakati wa mapambazuko.

29Mradi tumaini lake asiye na shukrani litayeyuka kama sakitu wakati wa baridi, na kwenda zake kama maji yasiyo na faida.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya