The chat will start when you send the first message.
1Lakini juu ya wale wabaya hasira iliwajia upeo bila huruma, kama vile yalivyojulikana yale yatakayowapata.
2Ndiyo ya kwamba, wakiisha kubadili nia zao ili kuwaachilia watu wako, na wakiisha kuwaharakisha waishike njia, wataghairi tena na kuwafuatia.
3Maana wale, hata walipokuwa katika kukaa matanga na kuomboleza panapo makuburi ya wafu wao, wakajivutia shauri lingine la upumbavu, na kuwafuatia kama watoro hao waliokwisha kuwatoa kwa kuwasihi.
4Mradi ajali iliyokuwa stahili yao ikiwaongoza hata mwisho huu, ikiwasahulisha mambo yale yaliyowajia, ili waitimilize adhabu mateso yao yaliyoikosa;
5tena watu wako waliposafiri kwa mapito ya ajabu, wale wenyewe waione mauti ya kigeni.
6Kwa maana ulimwengu mzima, kwa kadiri ya asili yake, ulifanyika tena mpya, kwa kuzitii amri zako hizi na hizi, ili watoto wako walindwe wasipatwe na dhara.
7Uwingu ulionekana uliokitia uvuli kituo chao, na nchi kavu ikapanda kutoka pale palipokuwapo maji kwanza, katika Bahari ya Shamu kukawa barabara isiyo na zuio, na uwanda wenye majani katika mawimbi yaumkayo.
8Hapo watu wako wakapita pamoja na majeshi yao yote, ambao kwa mkono wako walifunikwa, wakiisha kuona maajabu makuu.
9Wakazungukazunguka huru kama farasi, wakarukaruka kama wana-kondoo, wakikuhimidi Wewe, BWANA, uliyekuwa mkombozi wao.
10Wakati huo wakazidi kukumbuka mambo yale yaliyotokea hapo walipokuwa wakikaa hali ya kigeni, jinsi badala ya ng'ombe nchi ilizaa chawa, na badala ya samaki mto ulitoa wingi wa vyura.
11Hata baadaye wakaona na jamaa mpya ya ndege, hapo wakiongozwa na tamaa walipotaka vyakula vya anasa,
12na kwa kuwashibisha wakapewa kware kutoka bahari.
13Zaidi ya hayo, wale Wamisri wabaya wakajiliwa na adhabu, wakiisha kuonywa kwa dalili walizopewa katika nguvu za ngurumo; kwa sababu ilikuwa haki wateswe kwa ajili ya ubaya wao. Chuki ile waliyowafanyia wageni wao ilikuwa makuruhi zaidi,
14mradi watu wa Sodoma hawakuwakaribisha wageni walipowajia, bali Wamisri waliwafanya watumwa wageni wale waliowafaidia.
15Wala si hivyo tu, ila Mungu atawajia watu wa Sodoma namna nyingine kwa maana waliwapokea kama adui wale waliokuwa wageni;
16bali hao waliwakaribisha kwanza kwa karamu, na baadaye wakawatesa kwa kazi ngumu, watu waliokwisha kushirikiana nao katika haki za uraia.
17Na tena wakapigwa kwa kukosa kuona (kama vile wale wengine mlangoni pa Lutu, yule mtu wa haki) pindi walipozungukwa na giza tupu katika Misri wakatafuta kila mtu njia ya kuupitia mlango wake mwenyewe.
18Kwa kuwa ni kweli sauti za kinanda, zikibadili orodha yake zisibadilike zenyewe, zaweza kuutofautisha ulinganifu wa mwendo; vivyo hivyo yalivyofanya malimwengu ya asili kama ilivyoonekana kwa kutazama mambo yale yaliyotukia.
19Viumbe wakaao katika nchi kavu waligeuka viumbe vya majini, na viumbe vya kuogelea wakakanyaga ardhi;
20moto ukazidi upata nguvu katikati ya mvua, na maji yakasahau asili yake ya kuuzimisha;
21tena miali ya moto haikuunguza miili ya wanyama wapoteao waliotembea kati yake, wala katikati ya mvua, na maji yakasahau asili yake ya kuuzimisha; tena miali ya moto haikuunguza miili ya wanyama wapoteao waliotembea kati yake, wala haikuziyeyusha chembe za chakula kitamu, zilizofanana na barafu, na kuwa nyepesi za kuyeyuka.
22Wewe, BWANA, katika yote uliwakuza watu wako,
Ukawatukuza wala hukuwadharau,
Ukasimama upande wao kila wakati kila mahali.