Hekima ya Sulemani 2

Hekima ya Sulemani 2

1Maana walisemezana hivi, huku wakifikiri yasiyo kweli, Maisha yetu ni fupi yenye masumbufu, wala hakuna dawa ya kuponya iwapo binadamu aujia mwisho wake, wala hajajulikana mtu awezaye kufungua ahera.

2Tumezaliwa kwa bahati tu, hatimaye tutakuwa kana kwamba hatukupata kuwapo kamwe; mradi pumzi ya puani mwetu ni moshi, hata na akili ni cheche iliyowashwa kwa kupiga moyo wetu;

3ikizimika, mwili utageuka majivu, na roho itatoweka kama hewa.

4Halafu jina letu litasahauliwa, asizikumbuke kazi zetu hata mtu mmoja; na maisha yetu yatapita kama nyayo za wingu, yatatoweka kama ukungu, huku yakifukuzwa kwa vianga vya jua na kushindwa kwa moto wake.

5Siku zetu zi kama kivuli kipitacho, wala mwisho wetu hauahirishwi; kwa kuwa umetiwa mhuri, wala hakuna aurudishaye.

6Haya basi, njoni tujifurahishe kwa mema yaliyopo, tuvitumie vilivyoumbwa kwa roho yetu yote kama milki ya ujanani.[#Isa 22:13; 1 Kor 15:32]

7Tujishibishe kwa mvinyo ya thamani na manukato, wala ua lolote la demani lisitupite;

8tujivike taji za mawaridi kichwani kabla hayajanyauka;

9pasiwe na konde la majani tusipopiga ngoma zetu za anasa, na kila mahali tuziache dalili za machangamko yetu. Hilo ndilo fungu letu, na sehemu yetu ni hiyo.

10Hata tumwonee maskini mwenye haki; wala tusimhurumie mjane, wala tusimjali mzee mwenye mvi kwa sababu ya umri wake.

11Bali nguvu zetu zituwie sheria ya haki, kwa maana aliye dhaifu amebainika ya kuwa hana faida.

12Zaidi ya hayo na tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia kama tumeiasi torati, na kutushitaki kama tumekosa adabu.

13Asema ya kwamba anamjua Mungu, na kujiita mtumishi wa BWANA.

14Ametuwia magombezi ya fikira zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu;

15maana maisha yake si sawasawa na maisha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni.

16Tunahesabiwa naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Mwenye haki asema kuwa mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yao.

17Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake;

18mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake.

19Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa.

20Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.

Ujinga wa mwovu

21Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha;

22hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.

23Yaani, Mungu alimuumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe,[#Mwa 1:26-27]

24ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya