Hekima ya Sulemani 3

Hekima ya Sulemani 3

Mwisho wa mwenye haki

1Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa.

2Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwamba wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao,[#Hek 4:17]

3na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani.

4Kwa sababu hata ikiwa (waonavyo watu) wanaadhibiwa, hata hivyo taraja lao limejaa kutokufa,

5na wakiisha kustahimili kurudiwa kidogo watapokea wingi wa mema. Kwa kuwa Mungu amewajaribu, na kuwaona kuwa wamemstahili,[#Rum 8:18; 2 Kor 4:17]

6kama dhahabu katika tanuri aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara.

7Wakati wa kujiliwa kwao watang'aa, na kama vimulimuli katika mabua makavu watametameta.

8Watahukumu mataifa na kuwatawala makabila ya watu; naye BWANA atawamiliki milele na milele.

9Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake.

Mwisho wa wamchao Mungu

10Lakini wasio haki watalipwa kama vile walivyohojiana, ambao walimdharau mwenye haki na kumkosea BWANA;

11kwa maana mwenye kubeza hekima na malezi amekuwa duni. Na tumaini lao ni ubatili, wala kazi zao hazina faida, wala matendo yao hayafai kitu.

12Wake zao ni wapumbavu, na watoto wao ni wakorofi, hata kulaaniwa katika kuzaliwa kwao.

Heri mke tasa kuliko kizazi cha uovu

13Madhali yu heri yeye asiyezaa maadamu yu safi, hakuchukua mimba kwa kukosa; yeye atakuwa na matunda wakati ule Mungu atakapoangalia roho za watu.

Kuhusu wasiozaa

14Naye yu heri towashi ambaye hakutenda yasiyo sheria kwa mikono yake, wala hakuwaza maovu juu ya BWANA, mradi atapewa upendeleo kwa ajili ya uaminifu wake, na kura yake katika patakatifu pa BWANA itapendeza kuliko mke na watoto.

15Yaani, matendo mema yanayo matunda ya sifa njema, wala shina la ufahamu halikosekani.

16Bali watoto wa wazinzi hawawezi kupevuka, na wazao wa umalaya watatoweka.

17Hata wakiishi sana watahesabiwa kuwa ni hafifu, wala mwishowe uzee wao hautakua na heshima;

18tena wakifariki upesi hawana tumaini, wala hawatapata faraja siku ya neno mkataa.

19Kwa maana mwisho wa kizazi kisicho haki sikuzote ni mlemavu; basi, afadhali hali iliyo gumba pamoja na utakatifu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya