Sefania 2

Sefania 2

Hukumu kwa adui wa Israeli

1Jikusanyeni, naam, jikusanyeni, Ee taifa lisilo na haya;[#Yoe 2:16]

2kabla haijatolewa hiyo amri, kabla siku ile haijapita kama makapi, kabla haijawajia hasira kali ya BWANA, kabla haijawajia siku ya hasira ya BWANA.[#2 Fal 23:26]

3Mtafuteni BWANA, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya BWANA.[#Amo 5:6,15; Zab 76:9; Yoe 2:14]

4Kwa kuwa Gaza utaachwa, na Ashkeloni utakuwa ukiwa; wataufukuzia mbali Ashdodi wakati wa adhuhuri, na Ekroni utang'olewa.[#Yer 6:4; Isa 14:29-31; Yer 47:1-7; Eze 25:15-17; Yoe 3:4-8; Amo 1:6-8; Zek 9:5-7]

5Ole wao wakaao karibu na pwani ya bahari, taifa la Wakerethi! Neno la BWANA liko juu yenu, Ee Kanaani, nchi ya Wafilisti; mimi nitakuangamiza, asibaki mtu akaaye kwako.[#Eze 25:16; Yos 13:3]

6Na hiyo nchi ya pwani itakuwa malisho, yenye vibanda vya wachungaji, na mazizi ya makundi ya kondoo.[#Isa 17:2]

7Na hiyo nchi ya pwani itakuwa nchi ya watu wa nyumba ya Yuda waliosalia; watachunga makundi yao huko; watalala katika nyumba za Ashkeloni wakati wa jioni; kwa maana BWANA, Mungu wao, atawajia na kuwarudisha wafungwa wao.[#Isa 11:11; Hag 1:12; Mik 5:7; 4:10; Kut 4:31; Lk 1:68; Zab 126:4; Yer 23:3; Eze 39:25]

8Mimi nimeyasikia masuto ya Moabu, na dhihaka za wana wa Amoni, ambazo kwa hizo wamewatukana watu wangu, na kujitukuza juu ya mpaka wao. 21:28-32; 25:1-11; Amo 1:13-15[#Isa 15:1—16:14; 25:10-12; Yer 48:1—49:6; Eze]

9Basi kama niishivyo, asema BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, Hakika Moabu atakuwa kama Sodoma, na wana wa Amoni kama Gomora, yaani, milki ya upupu, na mashimo ya chumvi, ukiwa wa daima; watu wangu waliosalia watawateka nyara, na watu wa taifa langu waliobaki watawarithi.[#Isa 15:1; Amo 2:1; 1:13; Mwa 19:24]

10Mambo hayo yatawapata kwa sababu ya kiburi chao, kwa kuwa wamewatukana watu wa BWANA wa majeshi, na kujitukuza juu yao.

11BWANA atakuwa wa kutisha sana kwao; kwa maana atawaua kwa njaa miungu yote ya dunia; na watu watamsujudia yeye, kila mtu toka mahali pake; naam, nchi zote za mataifa.[#Mwa 49:10; 10:5; Zab 2:8; 22:27; Isa 2:2,3; 11:9,10; Mal 1:1; Yn 4:21; 1 Tim 2:8]

12Na ninyi Wakushi pia, mtauawa kwa upanga wangu.[#Isa 18:1-7]

13Naye atanyosha mkono wake juu ya upande wa kaskazini, na kuiangamiza Ashuru; naye ataufanya Ninawi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa.[#Isa 10:5-34; 14:24-27; Nah 1:1—3:19]

14Na makundi ya wanyama watalala kati yake, wanyama wote wa mataifa; bundi na kunguru watakaa juu ya vichwa vya nguzo zake; sauti yao itasikiwa madirishani; vizingitini mwake mtakuwa ukiwa; kwa maana ameifunua kazi ya mierezi.[#Isa 13:21]

15Huu ndio mji ule wa furaha,[#Isa 47:8; Ufu 18:7]

Uliokaa salama,

Uliosema moyoni mwake, Mimi niko,

Wala hapana mwingine ila mimi.

Jinsi ulivyokuwa ukiwa,

Mahali pa kulala pa wanyama wa bara!

Kila mtu apitaye atazomea,

Na kutikisa mkono wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya