1 Kor 2

1 Kor 2

Kumtangaza Kristo Aliyesulubiwa

1Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima.[#1 Kor 1:17]

2Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.[#Gal 6:14]

3Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi.[#Mdo 18:9; 2 Kor 10:1]

4Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu,

5ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.[#Efe 1:17; 1 The 1:5]

Hekima ya Kweli ya Mungu

6Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika;[#Flp 3:15]

7bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;[#Rum 16:25]

8ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;[#Lk 23:34; Yak 2:1; Kol 1:26]

9lakini, kama ilivyoandikwa,[#Isa 64:4]

Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia,

(Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,)

Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.

10Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.[#Mt 13:11; Mit 20:27]

11Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.

12Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.[#Yn 16:13,14]

13Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.[#1 Kor 1:4]

14Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.[#Yn 8:47; 14:17]

15Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.[#1 Yoh 2:20]

16Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.[#Isa 40:13; Rum 11:34]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania