1 Sam 7

1 Sam 7

1Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la BWANA, wakalileta ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la BWANA.[#2 Sam 6:2-4; 1 Nya 13:5-7; 1 Sam 6:21; Zab 132:6]

2Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea BWANA.

Samweli awa Mwamuzi

3Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti.[#Kum 30:2; 1 Fal 8:48; Isa 55:7; Hos 6:1; Yoe 2:12; Mwa 35:2; Yos 24:14; Amu 2:13; 2 Nya 30:19; Mt 4:10; 15:8; Lk 4:8]

4Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake.

5Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa BWANA.[#Amu 10:17; 11:11; 1 Sam 10:17; 2 Fal 25:23]

6Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.[#2 Sam 14:14; Neh 9:1,2; Dan 9:3; Yoe 2:12; Law 26:40; Amu 10:10; 1 Fal 8:47; Ayu 33:27,28; Zab 106:6]

7Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.

8Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.[#Isa 37:4]

9Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia.[#Zab 99:6; Yer 15:1]

10Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.[#Yos 10:10; Amu 4:15; 1 Sam 2:10; 2 Sam 22:14,15]

11Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari.

12Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa BWANA ametusaidia.[#1 Sam 4:1]

13Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli.[#Amu 13:1; 1 Sam 13:5]

14Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori.

15Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake.[#1 Sam 12:11; Amu 2:16]

16Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua Israeli mahali hapo pote.

17Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea BWANA madhabahu.[#Amu 21:4]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania