1 Tim 6

1 Tim 6

1Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.[#Efe 6:5; Tit 2:9,10]

2Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuonya.[#Flm 1:16]

Mafundisho ya Uongo na Utajiri Halisi

3Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa,[#Gal 1:6-9; 2 Tim 1:13]

4amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya;

5na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.[#2 Tim 3:8; 4:4; Tit 1:14]

6Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.[#1 Tim 4:8; Ebr 13:5; Flp 4:11,12]

7Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;[#Mhu 5:14; Ayu 1:21]

8ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.[#Mit 30:8]

9Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.[#Mit 23:4; 28:22]

10Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.[#Efe 5:5]

Vita Vizuri vya Imani

11Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.[#2 Tim 2:22]

12Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.[#1 Kor 9:25,26; 2 Tim 4:7]

13Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,[#Yn 18:36,37; 19:11]

14kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;

15ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;[#1 Tim 1:11; Ufu 17:14; Kum 10:17]

16ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.[#Kut 33:20]

17Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.[#Zab 62:10; Lk 12:20; Rum 12:16]

18Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo;

19huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.[#Mt 6:20]

Maagizo kwa Timotheo na Baraka

20Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo;[#1 Tim 4:7; 2 Tim 1:14]

21ambayo wengine wakiikiri hiyo wameikosa Imani. Neema na iwe pamoja nanyi.[#1 Tim 1:6; 2 Tim 2:18]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania