2 Kor 3

2 Kor 3

Wahudumu wa Agano Jipya

1Je! Tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji, kama wengine, barua zenye sifa kuja kwenu, au kutoka kwenu?[#2 Kor 5:12; Rum 16:1; Mdo 18:27]

2Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote;[#1 Kor 9:2]

3mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.[#Kut 24:12; 31:18; 34:1; Mit 3:3; 7:3; Rum 15:16; Yer 31:33; Eze 11:19; 36:26]

4Na tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo.

5Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.[#2 Kor 2:6]

6Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.[#Yer 31:31; 1 Kor 11:25; Rum 7:6; Yn 6:63]

7Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika;[#Kut 34:29]

8je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?[#Gal 3:2,5]

9Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.[#Kum 27:26; Rum 1:17; 3:21]

10Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana.[#Kut 34:29]

11Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu.

12Basi, kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi;

13nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika;[#Kut 34:33,35]

14ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo;[#Rum 11:25]

15ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao.

16Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.[#Kut 34:34; Rum 11:23,26]

17Basi “Bwana” ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.[#Yn 7:39; 8:36; Kut 16:7; 24:17; Rum 8:2]

18Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania