2 Sam 12

2 Sam 12

1Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.[#Zab 51:1; 2 Sam 14:5; 1 Fal 20:35; Mt 21:33,45; Lk 15:11]

2Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana;

3bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti.

4Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia.

5Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa;

6naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.[#Kut 22:1; Lk 19:8]

7Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli;[#1 Sam 16:13; 2 Sam 7:8]

8nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha.

9Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.[#Mwa 9:5,6; 1 Sam 15:19; Law 26:15,16; Hes 15:31; Mit 13:13; Isa 5:24; 2 Sam 11:15]

10Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.[#2 Sam 11:15]

11BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.[#2 Sam 16:22; Kum 28:30]

12Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.

13Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.[#1 Sam 15:24; 2 Sam 24:10; Ayu 7:20; Zab 32:5; 51:4; Mit 28:13; Zab 32:1; Mik 7:18; Zek 3:4]

14Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.[#Isa 52:5; Eze 36:20; Rum 2:24]

15Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake.[#Mwa 4:7; Amo 3:2]

Mtoto wa Bathsheba Afariki

Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana.

16Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini.[#Isa 26:16; Yer 18:8; 50:4; Amu 20:26; Yoe 1:14; 2 Sam 13:31]

17Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.

18Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?

19Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong’onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa.

20Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala.[#Rut 3:3; Ayu 1:20; Zab 95:6-8; 103:8-17; Mit 3:7; 16:6; Omb 3:40,41]

21Watumishi wake wakamwambia, Ni neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula.

22Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi?[#Isa 38:1,5; Yon 3:9]

23Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.[#2 Kor 5:1-8; Ebr 11:10; 13:14; Ayu 7:8,9]

Sulemani Azaliwa

24Naye Daudi akamfariji Bath-sheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda;[#Mt 1:6; 1 Nya 22:9]

25akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya BWANA.

Waamoni Waangamizwa

26Yoabu akapigana juu ya Raba wa wana wa Amoni, akautwaa mji wa kifalme.[#1 Nya 20:1; Kum 3:11]

27Yoabu akatuma wajumbe waende kwa Daudi, kusema Nimeshindana na Raba, hata nimeutwaa huo mji wa maji.

28Basi sasa kusanya watu waliobaki, ukauzunguke mji, na kuutwaa; nisije mimi nikautwaa mji, ukaitwe jina langu.

29Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa.

30Kisha akamnyang’anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nayo ilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana.[#1 Nya 20:2]

31Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya misumeno, na sululu za chuma, na mashoka ya chuma, akawatumikisha tanuuni mwa matofali; ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.[#12:31 Au, chini ya.]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania