2 Sam 24

2 Sam 24

Daudi Awahesabu Watu wa Israeli na Yuda

1Tena hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.[#2 Sam 16:10; 21:1; 1 Fal 22:22; 1 Nya 21:1; Yak 1:13; 1 Nya 27:23]

2Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu.[#Mwa 26:4; Kum 8:13,14; 2 Nya 32:25,26; Mit 18:12; 29:23; Yer 17:5]

3Naye Yoabu akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yo yote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme?

4Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli.[#1 Nya 21:4; Mhu 8:4; Mdo 5:29]

5Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kuume wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri;[#Kum 2:36; Hes 32:1,3]

6kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni,[#Yos 19:47; Amu 18:28,29; Yos 19:28]

7wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakatoka kusini kwa Yuda huko Beer-sheba.

8Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini.

9Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.[#1 Nya 21:5]

Hukumu ya Dhambi ya Daudi

10Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia BWANA, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee BWANA, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.[#1 Sam 24:5; Mit 18:4; 1 Yoh 3:20; 2 Sam 12:13; 1 Nya 21:8; Ayu 33:27,28; Zab 25:11; 1 Sam 13:13]

11Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la BWANA likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,[#1 Sam 22:5; 9:9]

12Nenda, ukanene na Daudi, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

13Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.[#1 Nya 21:12]

14Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.[#Zab 103:8; 119:156; Isa 47:6; Zek 1:15]

15Basi BWANA akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu.[#1 Nya 21:14; 27:24]

16Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa BWANA alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.[#Kut 12:23; 1 Nya 21:15; Zab 104:4; Mwa 6:6; 1 Sam 15:11; Zab 78:38; Yer 18:5-10; Yoe 2:13; Yon 3:10; 1 Nya 21:15; #24:16 Au, Ornani.]

17Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na BWANA, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.[#1 Nya 21:17]

Madhabahu ya Daudi katika Kiwanja cha Kupuria

18Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi.[#1 Nya 21:18]

19Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama BWANA alivyoamuru.

20Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi.

21Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.[#Mwa 23:8; Hes 16:48]

22Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng’ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe, viko kwa kuni,[#1 Fal 19:21]

23vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali.[#Zab 20:3; 119:108; Eze 20:40; 1 Pet 2:5]

24Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekeli hamsini za fedha.[#1 Nya 21:24]

25Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.[#1 Nya 21:28; 22:1; 2 Sam 21:14; 2 Nya 33:13; Isa 19:22]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania