2 The 2

2 The 2

Mtu wa Uvunjaji Sheria

1Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake,[#1 The 4:15-17]

2kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

3Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu;[#1 Tim 4:1; Yn 17:12; 1 Yoh 2:18; 4:3]

4yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.[#Dan 11:36; Eze 28:2]

5Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.[#Mdo 20:29]

8Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;[#Isa 11:4; Ayu 4:9; Ufu 19:15,20]

9yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;[#Mt 24:24; Ufu 13:11-13]

10na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.[#2 Kor 2:15; 4:3]

11Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;[#2 Tim 4:4]

12ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.

Waliochaguliwa kwa Wokovu

13Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli;[#Efe 1:4; Kum 33:12; 1 The 2:13; 4:7]

14aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.[#1 The 4:7; 5:9]

15Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu.

16Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema,[#1 The 3:11-13]

17awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania