The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme.
2Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo.
3BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA.[#Kum 32:36; Zab 106:45; 1 Nya 21:15; Hos 11:8; Yoe 2:14; Yon 3:10; Yak 5:16]
4Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukavila vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu.
5Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo.
6BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU.[#Zab 102:17]
7Haya ndiyo aliyonionyesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake.
8BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe;[#2 Fal 21:13; Isa 28:17; Mik 7:18]
9na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga.[#Mwa 26:23; 2 Fal 15:10]
10Ndipo Amazia, kuhani wa Betheli, akapeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote.[#1 Fal 12:32; 2 Fal 14:23]
11Kwa maana Amosi asema hivi, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake.
12Tena Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko;
13lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme.[#Amo 2:12]
14Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu;[#2 Fal 2:5; Zek 13:5]
15naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.
16Basi, sasa lisikie neno la BWANA; Wewe unasema, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka;[#Isa 30:10; Mik 2:6]
17kwa hiyo, BWANA asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.[#Yer 28:12; 29:21; Omb 5:11]