Amo 8

Amo 8

Kikapu cha Matunda

1Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa hari.

2Akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa hari. Ndipo BWANA akaniambia, Mwisho wao umewajilia watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe.[#Yer 1:12; Omb 4:18; Eze 7:2]

3Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya.

4Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi,

5mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu;[#Neh 13:15; Mik 6:10]

6tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano.

7BWANA ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.[#Zab 68:34; Hos 8:13]

8Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri.[#Hos 4:3; Amo 9:5]

9Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana.[#Ayu 5:14; Isa 13:10; Yer 15:9; Amo 4:13; Mik 3:6; 1 The 5:2,3]

10Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.[#Yer 6:26; Zek 12:10; Lk 7:12,13]

11Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA.[#1 Sam 3:1; Zab 74:9; Eze 7:26; Mik 3:6]

12Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione.

13Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.

14Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.[#Kum 9:21; 1 Fal 12:30; Hos 8:5,6; 10:5; Mik 1:5]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania