Amo 9

Amo 9

Kuangamizwa kwa Israeli

1Nalimwona Bwana akisimama karibu na madhabahu; akasema, vipigo vichwa vya nguzo, hata vizingiti vitikisike; vivunje vipande vipande juu ya kichwa cha kila mmoja wao; nami nitamwua mtu wa mwisho wao kwa upanga; hapana hata mmoja wao atakayekimbia, wala hataokoka hata mmoja wao.

2Wajapochimba waingie katika kuzimu, mkono wangu utawatoa huko; nao wajapopanda hata mbinguni, nitawatelemsha toka huko.[#Zab 139:8; Ayu 20:6; Oba 1:4]

3Nao wajapojificha katika kilele cha Karmeli, nitawatafuta na kuwatoa toka huko; na wajapositirika katika vilindi vya bahari nisiwaone, nitamwagiza joka huko, naye atawauma.[#Yer 23:24]

4Nao wajapokwenda hali ya kufungwa mbele ya adui zao, nitauagiza upanga huko, nao utawaua; nami nitawaelekezea macho yangu niwatende mabaya, wala si mema.[#Kum 28:65; Law 17:10]

5Kwa maana Bwana, MUNGU wa majeshi, ndiye aigusaye nchi, nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani yake wataomboleza; nayo itainuka yote pia kama Mto, nayo itakupwa tena kama Mto wa Misri.[#Mik 1:4]

6Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA ndilo jina lake.

7Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri?[#Kum 2:23; Yer 47:4; Amo 1:5]

8Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA.[#Zab 11:4; Yer 30:11]

9Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini.

10Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele.

Kurudishwa kwa Ufalme wa Daudi

11Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;[#Mdo 15:16-18]

12wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo.[#Oba 1:19; Hes 24:18]

13Angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka.[#Law 26:5]

14Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake.[#Isa 61:4]

15Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang’olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema BWANA, Mungu wako.[#Isa 60:21]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania