Kum 7

Kum 7

Watu Wateule wa Bwana

1BWANA, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang’oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe;[#Mdo 13:19]

2wakati BWANA, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao;[#Yos 6:17; 11:11; Kut 23:32; Yos 2:14; Amu 1:24; 2:2]

3binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake.[#Yos 23:12; 1 Fal 11:2; Ezr 9:2]

4Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi.

5Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.[#Kum 12:3; Kut 23:24; 34:13]

6Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako; BWANA Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.[#Kut 19:5; Kum 4:20; 14:2; 26:18; Tit 2:14; 1 Pet 2:9; Zab 50:5; Yer 2:3; Amo 3:2; 1 Kor 6:19,20; Zab 135:4]

7BWANA hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote;

8bali kwa sababu BWANA anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu BWANA akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.[#Kut 32:13; Zab 105:8; Lk 1:55; Kut 13:3]

9Basi jueni ya kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;[#Kut 20:5-6; 34:6-7; Hes 14:18; Kum 5:9-10; Isa 49:7; 1 Kor 1:9; 10:13; 2 Kor 1:18; 1 The 5:24; 2 Tim 2:13; Ebr 11:11; 1 Yoh 1:9; Neh 1:5; Dan 9:4]

10naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake.[#Zab 21:8; Mit 11:31; Isa 59:18; Nah 1:2; Rum 12:19]

11Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende.

Baraka za Utiifu

12Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi BWANA, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;[#Kum 11:13-17]

13naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng’ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.[#Kut 23:25; Zab 1:3; 11:7; Mit 15:9; Yn 14:21; 1 Yoh 2:5]

14Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo.

15Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.[#Kut 9:14; 15:26; Kum 28:27; Zab 105:37]

16Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa BWANA, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.[#Amu 8:27; Zab 106:36]

17Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?[#Hes 33:53]

18Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;[#Amu 6:13; Zab 77:11; 105:5; 135:8-10; Isa 63:11-15]

19uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.

20Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.[#Kut 23:28; Yos 24:12]

21Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.[#Hes 14:9; 16:3; Yos 3:10; Kum 10:17; Neh 1:5; 4:14; 9:32]

22Naye BWANA, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu.

23Ila BWANA, Mungu wako, atawatoa mbele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa.

24Na wafalme wao atakutilia mkononi mwako, nawe utalipoteza jina lao litoke chini ya mbingu; hapana mtu atakayeweza kusimama mbele yako, hata utakapokwisha kuwaangamiza.[#Yos 10:24; 12:1; Kum 11:25; Yos 1:5; 10:8; 23:9]

25Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako;[#Kut 32:20; Kum 12:3; 1 Nya 14:12; Kut 20:17; Yos 7:1; Lk 12:15; Kol 3:5; Amu 8:27; Sef 1:3; Kum 17:1]

26na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.[#Law 27:28; Yos 6:17]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania