The chat will start when you send the first message.
1Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia;[#Est 8:12; 3:13; 2 Sam 22:41; Isa 14:2]
2siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa hofu yao imewaangukia watu wote.[#Est 8:11,17; Zab 71:13; Kut 23:27]
3Nao maakida wa majimbo, na majumbe, na maliwali, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; kwa sababu hofu ya Mordekai imewaangukia.[#Mit 16:7]
4Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika majimbo yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa.[#2 Sam 3:1; 1 Nya 11:9; Zab 1:3; Mit 4:18; Isa 9:7]
5Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia.
6Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza.
7Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha,
8na Poratha, na Adalia, na Aridatha,
9na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha,
10wana kumi wa Hamani bin Hamedatha, adui ya Wayahudi; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.[#Kut 20:5; Est 5:11; Ayu 18:19; Zab 21:10; Mwa 14:14-16; Est 8:11]
11Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Shushani ngomeni.
12Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa.
13Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule.[#2 Sam 21:6,9]
14Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani.
15Basi Wayahudi wa Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Shushani; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
16Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu sabini na tano elfu; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.[#Law 26:7,8; 1 The 5:22]
17Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
18Lakini Wayahudi wa Shushani walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
19Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na boma, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi.[#Kum 16:11,14; Zab 118:15; Ufu 11:10; 1 Sam 25:8; Neh 8:10-12; Est 8:17]
20Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali,
21kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka,[#Zab 145:4]
22ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini vipawa.[#Zab 30:11; Mt 5:4; Yn 16:20-22; Mdo 2:44-46]
23Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia;
24kwa sababu Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia;[#Est 3:6,7]
25bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba hilo shauri baya alilolifanya juu ya Wayahudi limrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti.[#1 Sam 24:12,13; Est 7:10; Zab 7:16; 37:12,13]
26Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowajia,
27Wayahudi wakaagiza na kutadariki juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, na juu ya wote watakaojiunga nao, isikome, ya kwamba watazishika siku hizo mbili sawasawa na andiko lile, na kwa majira yake kila mwaka;[#Est 8:17; Isa 56:3,6; Zek 2:11]
28siku hizo zikumbukwe na kushikwa kwa vizazi vyote na kila jamaa, katika kila jimbo na kila mji; wala siku hizo za Purimu zisikome katikati ya Wayahudi, wala kumbukumbu lake lisiishe kwa wazao wao.
29Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu.[#Est 2:15; 8:10]
30Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia na ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli,
31ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, kwa habari ya kufunga na kilio.
32Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu.