Kut 19

Kut 19

Wana wa Israeli Waufikia Mlima wa Sinai

1Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai.

2Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.

3Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;[#Mdo 7:38]

4Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.[#Kum 32:11; Isa 63:9; Ufu 12:14]

5Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,[#Kum 4:20; 7:6; 10:14; 14:2; 26:18; 32:8; 1 Fal 8:53; Zab 50:12; 135:4; Tit 2:14; 1 Kor 10:26]

6nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.[#Ufu 1:6; 5:10; 20:6; 1 Pet 2:5,9; Law 20:24; Kum 7:6; Isa 62:12; 1 The 5:27]

7Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza.

8Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.[#Kut 24:3,7; Kum 26:17]

Watu Watakaswa

9BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia BWANA hayo maneno ya watu.[#Kum 4:11,12; Zab 97:2; Mt 17:5; Yn 12:29]

10BWANA akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,[#Ebr 10:22; Law 15:5]

11wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.[#Kut 34:5; Kum 33:2]

12Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.[#Ebr 12:18-20]

13Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima.

14Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.

15Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.[#1 Kor 7:5]

16Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.[#Ufu 4:5]

17Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima.[#Kum 4:10]

18Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu BWANA alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.[#Amu 5:5; Zab 68:7,8; 2 Nya 7:1; Mwa 15:17; Ufu 15:8; Yer 4:24]

19Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.[#Neh 9:13; Zab 81:7]

20BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.

21Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.[#1 Sam 6:19]

22Makuhani nao, wamkaribiao BWANA, na wajitakase, BWANA asije akawafurikia.[#Law 10:3; 2 Sam 6:7]

23Musa akamwambia BWANA, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga.

24BWANA akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia BWANA, asije yeye akawafurikia juu yao.

25Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania