Kut 24

Kut 24

Damu ya Agano

1Kisha BWANA akamwambia Musa, Kweeni wewe, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini wa wazee wa Israeli, mkamfikilie BWANA; mkasujudie kwa mbali;[#Kut 28:1; Law 10:1,2; Hes 11:16]

2na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na BWANA; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye.

3Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda.

4Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,[#Kum 31:9; Mwa 28:18; 31:45]

5akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe.

6Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu.[#Ebr 9:18]

7Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii.

8Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote.[#Mt 26:28; Mk 14:24; Lk 22:20; 1 Kor 11:25; 1 Pet 1:2; Ebr 9:19-20; 10:29]

Juu ya Mlima: Utukufu wa Mungu Waonekana

9Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli;

10wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake.[#Mwa 32:30; Kut 3:6; 33:20,23; Isa 6:1,5; Yn 1:18; 1 Tim 6:16; 1 Yoh 4:12; Eze 1:26; 10:1; Ufu 4:3; Mt 17:2]

11Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.[#Kut 19:21; Mwa 16:13; Kum 4:33; Mwa 31:54; Kut 18:12]

12BWANA akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe.[#Kut 32:15; Kum 5:22]

13Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu.[#Kut 33:11]

14Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee.

15Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima.[#Kut 19:9; Mt 17:5]

16Na huo utukufu wa BWANA ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu.[#Kut 16:10; Hes 14:10]

17Na kuonekana kwake ule utukufu wa BWANA kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli.[#Ebr 12:18]

18Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku.[#Kum 9:9]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania