Kut 33

Kut 33

Agizo la Kuondoka Sinai

1BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii;[#Mwa 12:7; 26:3; 28:13]

2nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi;[#Kum 7:22; Yos 24:11]

3waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia.[#Kut 32:9; Kum 9:6]

4Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri.[#2 Sam 19:24]

5BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda.[#Zab 139:23]

6Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele.

Hema nje ya Kambi

7Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa BWANA, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago.[#2 Sam 21:1]

8Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani.[#Hes 16:27]

9Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa.[#Zab 99:7]

10Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.

11Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.[#Mwa 32:30; Kum 5:24; 34:10; Kut 24:13]

Maombezi ya Musa kwa Mungu

12Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.[#Zab 1:6; Yer 1:5; Yn 10:14; 2 Tim 2:19]

13Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.[#Kut 34:9; Zab 25:4; 27:11; Kum 9:26; Yoe 2:17]

14Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.[#Kut 40:34-38; Isa 63:9; Kum 3:20; Yos 21:44; 22:4; 23:1; Zab 95:11]

15Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.[#Kut 34:9]

16Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?[#Hes 14:14; Kum 4:34; 2 Sam 7:23; Zab 147:20; Tit 2:14]

17BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.[#Mwa 19:21; Yak 5:16]

18Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako.[#1 Tim 6:16]

19Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.[#Rum 9:1,15; 4:4; Yer 31:14]

20Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.[#Mwa 32:30; Kum 5:24; Amu 13:22; Isa 6:5; Ufu 1:16]

21BWANA akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba;

22kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita;[#Isa 2:21; Zab 91:1,4]

23nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.[#Yn 1:18; 1 Tim 6:16; 1 Yoh 4:12]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania