Kut 38

Kut 38

Kutengeneza Madhabahu ya Sadaka za Kuchomwa

1Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu.[#Kut 27:1; 2 Nya 29:23,24; Zab 51:15-19; Isa 61:8; Eze 44:11; 45:17; Ebr 9:14; 13:10]

2Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba.

3Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba.[#1 Fal 7:45]

4Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu.

5Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia.

6Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba.

7Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao.

8Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.[#Kut 30:18; 2 Fal 16:17; 2 Nya 4:2; Zab 26:6; Zek 13:1; Eze 36:25; 2 Kor 7:1; Ebr 10:22; 1 Yoh 5:6]

Kutengeneza Behewa la Sanduku la Agano

9Naye akafanya ule ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua ya ua ilikuwa ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia;[#Kut 27:9; Zab 84:2; 92:13]

10nguzo zake zilikuwa ishirini, na matako yake yalikuwa ishirini, yalikuwa ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

11Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia vivyo, nguzo zake ishirini na matako yake ishirini, yalikuwa ni ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

12Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na matako yake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

13Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini.

14Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na matako yake matatu;

15ni vivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na matako yake matatu.

16Chandarua za nguo zote za ule ua zilizouzunguka pande zote zilikuwa za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa.

17Na matako ya zile nguzo yalikuwa ya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha.

18Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wake dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua.[#2 Nya 3:14]

19Na nguzo zake zilikuwa nne, na matako yake manne, yalikuwa ya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

20Na vigungi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba.[#Kut 27:19; 2 Nya 3:9; Ezr 9:8; Isa 22:23; Efe 2:21,22]

Kutengeneza Behewa la Sanduku la Agano

21Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani.[#Hes 1:50; 9:15; 18:2; 2 Nya 24:6; Mdo 7:44; Hes 4:28,33]

22Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda, akafanya yote BWANA aliyomwagiza Musa.[#Kut 31:2,6]

23Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri.

24Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na kenda, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu.[#Kut 30:13; Law 5:15; 27:3,25; Hes 3:47; 18:16]

25Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu;[#Kut 30:11-16]

26kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya watu waume sita mia na tatu elfu, na mia tano na hamsini (603,550).[#Mt 17:24; Kut 30:13,15; Hes 1:46]

27Na hizo talanta mia za fedha zilikuwa kwa kusubu yale matako ya mahali patakatifu na matako ya hilo pazia; matako mia kwa hizo talanta mia, talanta moja tako moja.[#Kut 26:19-32]

28Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake.

29Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne.

30Naye akafanya ya hiyo shaba matako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu,

31na matako ya ua kuuzunguka pande zote, na matako ya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.[#Kut 27:19; 2 Nya 3:9; Ezr 9:8; Isa 22:23; Efe 2:21,22]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania