Eze 41

Eze 41

1Akanileta mpaka hekaluni, akaipima miimo, upana wake dhiraa sita upande mmoja, na upana wake dhiraa sita upande wa pili, ambao ulikuwa ni upana wa maskani.[#Zek 6:12; Mt 16:18; 1 Kor 3:16; 2 Kor 6:16; Efe 2:21; Ufu 3:12]

2Na upana wa maingilio yake ulikuwa dhiraa kumi; na mbavu za maingilio zilikuwa dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; akaupima urefu wake, dhiraa arobaini, na upana wake, dhiraa ishirini.

3Kisha akaingia ndani, akapima kila mwimo wa maingilio, dhiraa mbili; nayo maingilio, dhiraa sita; na upana wa maingilio dhiraa saba.

4Akaupima urefu wake; dhiraa ishirini, na upana wake, dhiraa ishirini, mbele ya hekalu; akaniambia, Hapa ndipo mahali patakatifu kuliko kila mahali.[#1 Fal 6:20; 2 Nya 3:8; Ufu 21:2,3,16,17]

5Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote.

6Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba.[#1 Fal 6:5,6]

7Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati.

8Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita.[#Isa 28:16; Eze 40:5]

9Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba,

10na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote.

11Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote.

12Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini.

13Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia; na mahali pale palipotengeka na jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia;

14tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki, dhiraa mia.

15Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia; na hekalu la ndani, na kumbi za ua;

16na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za orofa zile tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hata madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa);[#1 Fal 7:4; Isa 54:12; Eze 40:16; 1 Kor 13:12]

17na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje,

18kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili;[#Mwa 3:24; Kut 25:22; 1 Sam 4:4; 2 Sam 22:11; 1 Fal 6:29; 2 Nya 3:10; Zab 80:1; 99:1; Eze 10:2,14; 1:10; Ufu 4:7-9]

19basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote.

20Toka chini hata juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi ukuta wa hekalu.

21Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza.

22Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii ndiyo meza iliyo mbele za BWANA.[#Kut 30:1,8; 1 Fal 7:48; 2 Nya 4:19; Ufu 8:3; Mit 9:2; Wim 1:12; Eze 44:16; Mal 1:7,12]

23Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili.[#1 Fal 6:31-35]

24Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili.

25Na milango ya hekalu ilifanyiziwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta zilivyofanyiziwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje.

26Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu, katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya boriti zile nene.[#Eze 40:16]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania