Eze 5

Eze 5

Upanga dhidi ya Yerusalemu

1Nawe, mwanadamu, ujipatie upanga mkali, kama wembe wa kinyozi ujipatie, ukaupitishe juu ya kichwa chako na ndevu zako; kisha ujipatie mizani ya kupimia, ukazigawanye nywele hizo.[#Law 21:5; Isa 7:20; Eze 44:20]

2Theluthi ya hizo utaiteketeza katikati ya mji, siku za mazingiwa zitakapotimia; nawe utatwaa theluthi, na kuipiga kwa upanga pande zote; nawe utatawanya theluthi ichukuliwe na upepo, nami nitafuta upanga nyuma yake.[#Eze 4:1]

3Nawe twaa nywele chache katika hizo, na kuzifunga katika upindo wa mavazi yako.[#Yer 40:6]

4Nawe utatwaa tena baadhi ya hizo, na kuzitupa katikati ya moto, na kuziteketeza katika moto huo; kutoka nywele hizo moto utakuja na kuingia katika nyumba yote ya Israeli.[#Yer 41:1,2]

5Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio Yerusalemu; nimeuweka kati ya mataifa, na nchi zauzunguka pande zote.

6Nao umeasi hukumu zangu, kwa kutenda mabaya kuliko mataifa hayo, nao umeasi sheria kuliko nchi hizo ziuzungukazo; maana wamezikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika sheria zangu.[#Rum 1:25; Yud 1:4]

7Basi, kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi mmefanya ghasia kuliko mataifa wawazungukao ninyi, wala hamkuenda katika sheria zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, wala hamkutenda kama kawaida za mataifa wawazungukao;[#Yer 2:10; Eze 11:12]

8basi, Bwana MUNGU asema hivi; Angalia, mimi, naam, mimi, ni juu yako; nami nitafanya hukumu kati yako machoni pa mataifa.

9Nami nitakutenda nisiyoyatenda zamani, wala sitafanya tena mambo kama hayo, kwa sababu ya machukizo yako yote.[#Omb 4:6; Dan 9:12; Amo 3:2; Mt 24:21]

10Kwa sababu hiyo baba za watu watawala wana wao kati yako, nao wana watawala baba zao; nami nitafanya hukumu ndani yako, na hao wote waliosalia kwako nitawatawanya kwa pepo zote.[#Kum 28:53; Yer 19:9; Omb 2:20; 4:10; Law 26:33; Eze 12:14]

11Kwa sababu hiyo, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa kuwa umepatia unajisi patakatifu pangu, kwa matendo yako yote niyachukiayo, na kwa machukizo yako yote, kwa sababu hiyo mimi nami nitakupunguza; wala jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma.[#2 Nya 36:14; Eze 7:20; 11:21]

12Theluthi yenu mtakufa kwa tauni, na kwa njaa watakomeshwa ndani yako; na theluthi yenu wataanguka kwa upanga pande zako zote; na theluthi yenu nitawatawanya kwa pepo zote, kisha nitafuta upanga nyuma yao.[#Yer 15:2; 9:16; Eze 6:8,12; 12:14]

13Hivyo ndivyo ghadhabu yangu itakavyotimia, nami nitatosheleza hasira yangu juu yao, nami nitafarijika; nao watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimenena kwa wivu wangu, nitakapokuwa nimeitimiza ghadhabu yangu juu yao.[#Omb 4:11; Dan 9:2; Kum 32:36; Isa 1:24]

14Tena nitakufanya kuwa ukiwa, na aibu, kati ya mataifa wakuzungukao, machoni pa watu wote wapitao.[#Law 26:31; Neh 2:17]

15Nayo itakuwa tukano na aibu, na mafundisho na ajabu, kwa mataifa wakuzungukao, hapo nitakapotekeleza hukumu ndani yako, kwa hasira, na kwa ghadhabu, na kwa malaumu ya ghadhabu; mimi, BWANA, nimeyanena hayo;[#Kum 28:37; Zab 79:4; Yer 24:9; Omb 2:15; 1 Kor 10:11; Eze 25:17]

16hapo nitakapopeleka mishale mibaya ya njaa juu yao, iletayo uharibifu, nitakayoipeleka ili kuwaharibu ninyi; nami nitaiongeza njaa juu yenu, na tegemeo lenu la mkate nitalivunja.[#Kum 32:23,24; Eze 14:21]

17Nami nitapeleka juu yenu njaa na wanyama wabaya, nao watakunyang’anya watu wako; na tauni na damu zitapita ndani yako; nami nitauleta upanga juu yako; mimi BWANA, nimeyanena hayo.[#Law 26:22; Eze 38:22; Ufu 6:8]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania