Mwa 17

Mwa 17

Ishara ya Agano

1Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu.[#Mwa 5:22; Ayu 1:1]

2Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.[#Gal 3:17,18]

3Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema,[#Kut 3:6]

4Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi,

5wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.[#Rum 4:17]

6Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako.

7Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.[#Lk 1:55; Mwa 26:24; 28:13; Ebr 11:16; Rum 9:7-9]

8Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.[#Mdo 7:5; Kut 6:7; 29:45; Law 26:12; Kum 4:37; 14:2; 26:18; Zab 48:14; Ufu 21:7]

9Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.[#Zab 25:10]

10Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.[#Mdo 7:8; Rum 4:11]

11Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.[#Mdo 7:8; Rum 4:11; Gal 6:15]

12Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.[#Lk 2:21; Yn 7:22]

13Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.

14Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.[#Kut 4:24; Yos 5:2-7]

15Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.

16Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake.[#Mwa 18:10; 21:1]

17Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?[#Mwa 18:12; 21:6,7]

18Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.

19Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake.[#Mwa 18:10; 21:2; Gal 4:28-31]

20Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.[#Mwa 16:10; 21:18; 25:12-16]

21Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao.[#Mwa 21:2]

22Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu.[#Mwa 18:33; 35:9-15]

23Ibrahimu akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote waliozaliwa nyumbani mwake, na wote walionunuliwa kwa fedha yake, wanaume wote wa watu wa nyumba ya Ibrahimu, akawatahiri nyama ya magovi yao siku ile ile, kama Mungu alivyomwambia.[#Mwa 17:9]

24Naye Ibrahimu alikuwa mwenye umri wa miaka tisini na kenda alipotahiriwa nyama ya govi lake.

25Na Ishmaeli mwanawe alikuwa mtu wa miaka kumi na mitatu, alipotahiriwa nyama ya govi lake.

26Siku ile ile akatahiriwa Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe.[#Zab 119:60]

27Na watu wote wa nyumba yake, wazaliwa nyumbani, na wanunuliwa kwa fedha katika mkono wa mgeni, wakatahiriwa pamoja naye.[#Mwa 14:14; 18:19]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania