The chat will start when you send the first message.
1BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema.[#1 Sam 2:21; Mwa 17:19; 18:10; Gal 4:23]
2Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.[#Ebr 11:11; Mdo 7:8]
3Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia.[#Mwa 17:19]
4Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.[#Mwa 17:12; Mdo 7:8]
5Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka.
6Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami.[#Zab 126:2; Isa 54:1; Lk 1:14,58]
7Akasema, N’nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.[#Mwa 18:11]
8Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya.
9Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.[#Mwa 16:1,4,15; Gal 4:29]
10Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.[#Gal 4:29-30; Mwa 25:6; 36:6,7]
11Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.[#Mwa 17:18]
12Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.[#Rum 9:7; Ebr 11:18]
13Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.[#Mwa 16:10; 17:20; 25:12]
14Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.[#Yn 8:35]
15Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.[#Hes 20:5; Zab 63:1]
16Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.[#Mwa 44:34]
17Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.[#Kut 3:7; 2 Fal 13:4,23]
18Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.[#Mwa 21:13; 25:12; Amu 8:24]
19Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.[#Hes 22:31; 2 Fal 6:17; Lk 24:16]
20Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.[#Mwa 16:12; 39:2,3]
21Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.[#Mwa 24:4; 20:2; 26:28; Isa 8:10]
22Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.[#Mwa 26:26]
23Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake.[#Yos 2:12; 1 Sam 24:21]
24Ibrahimu akasema, Nitaapa.
25Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang’anya.[#Mwa 26:15-22]
26Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu.
27Ibrahimu akatwaa kondoo na ng’ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano.[#Mwa 26:28-31]
28Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao.
29Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini?[#Mwa 33:8]
30Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki.[#Mwa 31:48]
31Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili.[#Mwa 26:33]
32Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti.[#Yos 13:2]
33Ibrahimu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la BWANA Mungu wa milele.[#Kum 33:27; Zab 9:7; Isa 9:6; Rum 16:26; Ebr 13:8; 1 Tim 1:17; Ufu 10:6]
34Ibrahimu akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.